Libya: Gutteres asema vituo vya kuwazuia wahamiaji vifungwe
4 Septemba 2020Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiafa Antonio Guterres amesema hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha hali mbaya ya wakimbizi na wahamiaji wanaozuiliwa nchini Libya. Guterres ameitaka mamlaka ya Libya kutimiza majukumu yake chini ya sheria za kimataifa na kuvifunga vituo vyote kwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya Umoja wa Mataifa. Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya watu 2,780 walizuiliwa nchini Libya hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Julai katika vituo hivyo.
Asilimia 22 ya wafungwa walikuwa watoto. Guterres amesisitiza kwamba watoto hawapaswi kuwekwa mahabusu kamwe, haswa wanapokuwa wametenganishwa na wazazi wao na ameihimiza serikali ya Libya juu ya kuwalinda watoto mpaka pale suluhisho la muda mrefu litakapopatikana.
Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia imenukuu mateso, kutoweka kwa watu, unyanyasaji na kuwadhulumu watu kingono katika vituo hivyo. Guterres alitaja pia ukosefu wa chakula na huduma za afya. Ripoti hiyoimetaja visa vya wanaume ambao mara kwa mara wanatishiwa na kulazimishwa kuwapigia simu familia zao, na kuwashinikiza watume fedha za fidia kwa makundi yanayowazuia.
Ripoti hiyo imesema baadhi ya wahamiaji na wakimbizi wamepigwa risasi wakati walipojaribu kutoroka, hali ambayo imesababisha majeraha na hata vifo. Baadhi ya wakimbizi na wahamiaji hufanyishwa kazi kwa nguvu katika sehemu za kuhifadhia silaha ambapo wanalazimika kuzikarabati au kuzishughulikia silaha zinazotumiwa na makundi yasiyotii sheria imesema ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu shambulio la anga lilipofanyika mnamo mwezi Julai mwaka 2019 ambapo zaidi ya wakimbizi 50 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa katika kituo cha kuwazuia wahamiaji karibu na mji wa Tripoli, na hadi sasa hakuna mtu aliyewajibishwa na uovu huo.
Libya imekuwa katika machafuko tangu kuondolewa madarakani na kuuawa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gadaffi mnamo mwaka 2011. Makundi yanayopingana yanagombea madaraka. Libya imegeuka kuwa njia kuu inayotumiwa na wahamiaji haramu wanaotaka kwenda bara Ulaya, kupitia bahari ya Mediterania.
Chanzo:/AFP
2020-09-03T20:18:12Z UTC