Libya yakubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
9 Oktoba 2015Bernardino Leon ameuambia mkutano wa waandishi wa habari jana jioni nchini Morocco kuwa majina ya wagombea watakaoongoza katika serikali ya umoja wa kitaifa tayari yameamuliwa.
Tangazo hilo ni hatua muhimu ya kuiunganisha nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta lakini iliyosambaratika baada ya kuangushwa kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka wa 2011. Tangu wakati huo nchi imegawika baina ya serikali inayoungwa mkono na wanamgambo yenye makao yake mjini Tripoli na serikali inayotambulika kimataifa yenye makao yake mashariki mwa nchi.
Wapatanishi walioshiriki mazungumzo ya amani kwa niaba ya serikali zao pinzani waliyaidhinisha majina ya wagombea, lakini mabunge ya pande zote mbili lazima yayaidhinishe pia.
Haikubainika haraka ikiwa kambi zote zinaunga kono orodha ya wagombea, hasa wakati serikali yenye makao yake mjini Tripoli ikiwa imepasuka baina ya viongozi wenye msimamo mkali na wa wastani. Leon amesema waziri mkuu aliyependekezwa kuongoza serikali mpya ni Fayez Sarraj, mwanachama wa bunge lenye makao yao mjini Tripoli.
Mussa al-Kouni, mmoja wa viongozi waliopendekezwa kupewa wadhifa wa naibu waziri mkuu amesema sehemu ngumu sasa imeanza. Naima Jibril, jaji na mwanachama wa Tume ya Kitaifa ya Maridhiano amesifu kujumuishwa kwa mawaziri wanawake wawili katika orodha hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezikaribisha habari hizo, akiyaomba kambi zote mbili kusaini muafaka huo. Mikataba ya awali ya kusitisha mapigano na kurejesha utulivu katika nchi hiyo imesambaratika na maafisa kutoka pande zote mbili za mgogoro huo wameelezea mashaka yao kuhusiana na tangazo la Leon
Serikali mpya ya umoja wa kitaifa ina changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uchumi unaokaribia kuporomoka, makundi kadhaa ya wapiganaji na mahitaji makubwa ya msaada muhimu. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 2.5 nchini Libya, ambao ni karibu asilimia 40 ya jumla ya idadi ya watu nchini humo – wanahitaji ulinzi na aina Fulani ya msaada wa kiutu.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Sessanga