Ligi ya mabingwa wa dunia yaanza rasmi Bayern kidedea
23 Agosti 2014Pambano hilo lilifanyika katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich jana usiku. Arjen Robben na Thomas Muller ndio waliopeleka furaha kwa mashabiki wa mabingwa hao watetezi Bayern Munich.
Mabingwa hao kutoka jimbo la Bavaria , wakiwakosa nusu ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza , walionesha kiwango cha juu kwa muda mfupi tu katika kipindi cha kwanza lakini ilitosha kuweza kunyakua pointi zote tatu muhimu mwanzoni mwa msimu huu.
Joachim Loew ashuhudia
Kocha wa mabingwa wa dunia Ujerumani, Joachim Loew alikuwapo katika pambano hilo, na kushuhudia Thomas Muller akiujaza wavuni mpira kwa pasi safi aliyomegewa na Arjen Robben katika dakika ya 37 baada ya mshambuliaji huyo wa pembeni kuwatoka walinzi wawili wa Wolfsburg.
Robben akaongeza bao la pili dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili, ambapo mshambuliaji wa Croatia Ivica Olic alifanikiwa kupunguza mwanya wa magoli kwa kupachika bao katika dakika ya 52 ya mchezo.
"Kwa kila kocha duniani ushindi ni kitu muhimu sana," Kocha wa Bayern Pep Guardiola amewaambia waandishi habari baada ya mchezo huo. Baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-0 hatukuweza kuudhibiti mchezo vizuri na tulikuwa na nguvu kwa muda wa dakika 65-70. Bado tunahitaji muda zaidi.
Guardiola aliendelea kutumia mbinu yake ya kuwatumia walinzi watatu licha ya kutokuwapo kwa wachezaji muhimu katika kikosi chake na alimtumia mlinzi Holger Badstuber ambaye amerejea tena uwanjani baada ya kuumia goti na kukaa nje ya uwanja kwa karibu miaka miwili.
"Tulifanya vizuri licha ya kutocheza na timu hii hapo kabla," mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani Badstuber amewaambia waandishi habari. Katika kipindi cha pili tulipungukiwa nguvu kidogo lakini kwa jumla ulikuwa mwanzo mzuri." Amesema Badstuber.
Ligi inaendelea
Ligi ya mabingwa wa dunia , Bundesliga inaendelea leo jioni (23.08.2014), ambapo makamu bingwa Borrusia Dortmund wanawakaribisha Bayer Leverkusen , na FC Koln iliyopanda daraja msimu huu inaoneshana kazi na Hamburg SV, timu ambayo ilikaribia kuiaga Bundesliga msimu uliopita na kunusurika kwa ncha ya kidole. Hertha BSC Berlin iko nyumbani ikiisubiri Werder Bremen , Eintracht Frankfurt ina miadi na Freiburg na Hannover wataoneshana kazi na Schalke 04. Hoffenheim watakuwa nyumbani kuwasubiri Augsburg, ambapo hapo kesho Jumapili (24.08.2014) itakuwa zamu ya wageni katika ligi hii Paderborn wakiwakaribisha Mainz 05 na kisha Gladbach watakamilisha ratiba ya kuanza kwa ligi ya Bundesliga wiki ya kwanza kwa kuikaribisha Stuttgart.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre
Mhariri: Yusuf ,Saumu