1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa wa Ulaya kukamilishwa Lisbon

Josephat Charo
17 Juni 2020

Mashindano ya kuwania kombe la mabingwa barani Ulaya, Champions, yatakamilika na mashindano ya siku 12 mjini Lisbon, Ureno kuanzia Agosti baada ya kusitishwa kutokana na janga la corona.

https://p.dw.com/p/3dvaI
UEFA Champions League | Benfica Lissabon – RB Leipzig
Picha: Getty Images/O. Passos

Timu nane zitacheza kuanzia mechi za robo fainali katika michezo ya mtoano kwenye viwanja viwili, kamati ya utendaji ya shirikisho la soka duniani FIFA imesema Jumatano (17.06.2020)

Mechi ya fainali itachezwa uwanja wa klabu ya Benfica Jumapili Agosti 23. Uamuzi wa kuyakamilisha mashindano hayo pia una maana uwanja wa Ataturk Olympic mjini Istanbul, ambao ulikuwa umechaguliwa kwa ajili ya fainali ya mwaka huu, sasa utatumika kwa fainali ya ligi ya mabingwa mwaka ujao.

Ligi ya Ulaya pia itakamilishwa kupitia mashindano ya timu nane katika mechi za mtoano zitakazochezwa katika viwanja vinne magharibi mwa Ujerumani kuanzia Agosti 1. Mji wa Cologne utakuwa mwenyeji wa fainali Ijumaa Agosti 21. Fainali hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa Mei 27 mjini Gdansk nchini Poland. Mji wa Gdansk sasa utaandaa fainali ya ligi ya Ulaya mwaka ujao 2021.

Mashindano ya kombe la mabingwa na ligi ya Ulaya hayajakamilisha mechi za robo fainali huku mechi za timu 16 bora zikisitishwa kutokana na janga la virusi vya corona. Hakuna uamuzi ulioafikiwa kuhusu wapi mechi hizo zitakakochezwa mapema mwezi Agosti.

Ligi ya mabingwa ina mechi nne za duru ya pili zilizoahirishwa mwezi Machi huko Barcelona, Bayern Munich, Juventus na Manchester City. Katika ligi ya Ulaya, mechi sita kati ya nane za duru ya kwanza ya timu 16 bora zilichezwa. Mechi moja moja zimeruhusiwa kuchezwa nchini Ujerumani kati ya Inter Milan na Getafe na Roma na Sevilla.

Mashindano ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA yamepangwa kuanza tena baada ya ligi za ndani kukamilika Agosti 23. Uamuzi mkubwa wakati wa sheria za kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya corona ulikuwa ule wa UEFA kuyaahirisha mashindano ya kombe la Ulaya EURO hadi Juni 2021. Miji yote 12 katika nchi 12 imethibitishwa tena Jumatano kuandaa mechi zao mwaka ujao.

(ap)