Ligi ya Ujerumani Bundesliga kuanza mwishoni mwa juma
14 Septemba 2020Ligi ya Ujerumani inarejea uwanjani mwishoni mwa juma hili, mchezo wa ufunguzi ukiwa siku ya Ijumaa tarehe 18.09 kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich wakiikaribisha Schalke 04 mara hii.
Lakini kabla ya kufunguliwa msimu wa ligi , kuanzia siku ya Ijumaa kumekuwa na michezo ya duru ya kwanza ya kombe la shirikisho DFB Pokal hapa Ujerumani, ambapo hadi jana timu pekee ya daraja la kwanza iliyoyaaga mashindano hayo ni Hertha BSC baada ya kutandikwa mabao 5-4 na Braunschweig.
Leo hii jioni ni zamu ya bingwa mtetezi Bayern Munich wakipambana na timu ya daraja la 4 Dueren, Borussia Dortmund itaoneshana kazi na timu ya daraja la tatu ya MSV Duisburg. Wakati Rot Weis Essen itakuwa mwenyeji wa Arminia Bielefeld, Hannover itakwaana na Wuezburger Kickers na Hamburg Sport Verein ina miadi na Dynamo Dresden.
Serikali kuu ya Ujerumani inaendelea na mtazamo wa uwiano wa nchi nzima kuhusiana na sheria wakati linakuja suala la kurejea kwa mashabiki katika viwanja vya michezo. Msemaji wa serikali Steffen Seibert alirudia leo azimio lililotolewa mwezi Agosti na kansela Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo nchini Ujerumani. Ilikubalika kuwa kikosi kazi kitateuliwa kuwasilisha mapendekezo na ushauri hadi mwishoni mwa Oktoba. Maelekezo ya mawaziri wakuu na kansela kwa kikosi kazi hicho bado yanatumika, alisema Seibert.
Ligi ya Ujerumani itaanza rasmi hapo Ijumaa tarehe 18, kati ya Bayern Munich na Schalke 04, mashabiki na wachambuzi wanatarajia nini katika msimu huu wa 57 wa Bundesliga.