Ligi za Ulaya kurejea uwanjani mwishoni mwa juma
12 Oktoba 2020Michezo katika ligi za nyumbani katika mataifa ya Ulaya inarejea viwanjani mwishoni mwa juma wakati msimu huu uliofanyiwa mabadiliko kutokana na janga la virusi vya corona ukiendelea kushika kasi. Nchini Ujerumani Bundesliga inarejea siku ya Jumamosi ambapo Mainz 05 inaikaribisha Bayer Leverkusen, Hoffenheim ina miadi na Borussia Dortmund, Augsburg ina kwaana na RB Leipzig, Hertha Berlin inatiana kifuani na VFB Stuttgart, wakati Werder Bremen inasafiri kwenda kupambana na Freiburg. Timu iliyopanda daraja msimu huu ya Arminia ina miadi na mabingwa watetezi Bayern Munich, wakati usiku kutakuwa na pambano kati ya Borussia Moenchengladbach ikiumana na VFL Wolfsburg.
Katika Premier League nchini England Everton inamiadi katika Meryeyside derby dhidi ya Liverpool, Chelsea inacheza na Southampton, Manchester City inapimana ubavu na Arsenal na Manchester United inasafiri kwenda Newcastle. Katika siku hiyo hiyo katika ligi ya Italia Serie A Juventus ni wageni wa Crotone, wakati viongozi wa ligi hiyo hivi sasa Atalanta inasafiri kwenda Napoli. Pia siku hiyo ya Jumamosi Real Madrid inawakaribisha Cadiz na barcelona inakibarua na Getafe katika La Liga nchini Uhispania.
Wakati huo huo katika kinyang'anyiro cha ligi ya mataifa ya Ulaya , Ujerumani itajaribu kuendeleza kile ilichofanya siku ya Jumamosi baada ya ushindi wake wa kwanza kuwahi kupata katika ligi hiyo, inaikaribisha Uswisi katika kundi A4, wakati viongozi wa kundi hilo Uhispania inasafiri kwenda Ukraine.
Baada ya mchezo kati ya Ujerumani na Ukraine kocha wa Ujerumani Joachim Loew alikuwa na haya ya kusema:
"Kwa ujumla nimefarijika, kwamba tulishinda mchezo huo. Nafikiri tungeweza bila shaka kabla ya goli tulilofungwa na Ukraine, kuongoza kwa mabao matatu au manne. Tulisababisha penalti ambayo haikuwa lazima. Kile kilichokuwa kizuri , ni kwamba tulifanikiwa kuwatoa nje ya mchezo Ukraine na kutoweza kabisa kutengeneza nafasi ya kupata bao."
Nae mchezaji wa ulinzi wa Ujerumani Matthias Ginter alikuwa na haya ya kusema kuhusu mchezo huo dhidi ya Ukraine:
"Nafikiri, kwamba tumefurahi, kwamba tumeshinda na kwamba ilikuwa muhimu kwa ajili ya kusonga mbele. Kwasababu ushindi ndio unasaidia, na hicho tumefanikiwa leo , lakini tunatambua pia, kwamba kwa sasa hatujacheza mchezo wa hali ya juu sana."
Siku ya Jumatano Italia itakuwa mwenyeji wa Uholanzi, Ufaransa ina ziara kwenda Croatia katika mchezo mwingine wa marudio wa fainali iliyopita ya kombe la dunia iliyofanyika mjini Moscow, na mabingwa wa kombe la ligi ya mataifa Ureno inawakaribisha nyumbani Sweden. England inakamilisha kipindi cha michezo ya kimataifa kwa kupambana na Denmark katika uwanja wa Wembley.
Lakini siku mbili baada ya Ujerumani kupambana na Uswisi, Bayern Munich tayari itakuwa na mchezo wake wa kwanza wa baada ya michezo ya kimataifa. Kocha Hans Flick atapata fursa ya kuwa ya kuwapumzisha wachezaji wanaorejea kutoka michezo ya kimataifa na kuwapa wachezaji wapya Eric Maxim Choupo-Moting, Bouna Sarr, Marc Roca na Douglas Costa nafasi katika kikosi kinachoanza na kupambana na Dueren katika mchezo wao wa kombe la Ujerumani DFB Pokal ulioahirishwa.
Mkutano wa kwanza wa kikosi kazi cha kitengo kinachoendesha ligi ya Ujerumani DFL kwa ajili ya mustakabali wa soka la kulipwa utafanyika kesho Jumanne katika moja kati ya makundi matatu, ambayo yana jumla ya wataalamu 35 kutoka katika makundi ya kisiasa, kijamii, sayansi na viwanja vya kandanda. Wawakilishi wa makundi ya mashabiki, ambayo yanadai mageuzi katika spoti, pia yatajiunga na mkutano huo. Kutokana na janga la virusi vya corona Bundesliga inakabiliwa na shinikizo kubwa la kifedha. Wakati huo huo kuna hofu ya uwezekano wa kugawiwa upya fedha pamoja na hatua nyingine za dharura ambazo zinaweza kuathiri uwezo wa vilabu katika mashindano ya kimataifa.