Lijue kundi linalojiita "Dola la Kiislam" (IS)
Kundi la IS lilianza kama kundi dogo baada ya kujitenga na al-Qaeda, na baadae kuwa kundi kubwa la kimataifa. DW inachunguza vipengele muhimu vya kundi hilo-kutoka utawala wa Kiislam hadi mbinu zake inazozitumia.
Lilianzia wapi?
Kundi linalojiita "Dola la Kiislam" (IS) - ambalo pia linajulikana kama ISIL au Daesh - limetokana na kundi lingine la al-Qaeda lenye itidaki za Kiislam za madhehebu ya Sunni. Limeibuka baada ya Marekani kuivamia Iraq 2003 na linaongozwa na Abu Bakr al-Baghdadi. Lengo lao ni kuleta utawala wa Kiislam duniani kote.
Linapatikana maeneo gani?
Inaaminika kundi la IS kuwa na kambi zake za operesheni katika zaidi ya nchi 12 duniani kote. Linadhibiti maeneo kadhaa nchini Iraq na Syria. Hata hivyo, kundi hilo limepoteza maeneo yake mengi Iraq na Syria mwaka 2014 wakati wa kilele chake.
Nani anaepambana na IS?
Marekani inaongoza muungano wa kimataifa wa zaidi ya nchi 50, zikiwano nchi kadhaa za Kiarabu. Urusi, Iran na kundi la Kishia la Lebanon la Hezbollah wote wanaiunga mkono serikali ya Syria ya Bashar al-Assad. Vikosi vya kikanda kama vile Kurdish peshmerga (kwenye picha) na wapiganaji wa Kikurdi wa Syria ambao wanaungwa mkono na Marekani. Wote hawa wanapigana na IS.
Vipi linajifadhili?
Vyanzo vikuu vya fedha kwa IS ni mafuta na gesi. Kuna wakati kundi hilo likidhibiti thuluthi moja ya mafuta yanayochimbwa Syria. Lakini baadae mashambulizi ya anga yaliyoongozwa na Marekani yalilenga visima hivyo vya mafuta. Na serikali ya Syria pamoja na wapiganaji wa Kikurdi wa Syria wakavikomboa visima hivyo. Njia nyingine ni kodi, malipo ya kukomboa mateka na kuuza vitu vya kihistoria.
Wapi linakofanya mashambulizi?
Kundi la IS limedai kuhusika na mashambulizi mengi ya kigaidi duniani kote. Kundi hilo limeshambulia miji mingi mikuu ya mataifa ya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Berlin, Brussels na Paris. IS pia linahamasisha wafuasi wake kufanya mashambulizi ya mtu mmoja bila ya kulihusisha moja kwa moja kundi hilo.
Inatumia njama gani nyingine?
Ili kujipanua, kundi la IS linatumia mikakati tofauti. Wapiganaji wa IS wamepora na kuharibu vitu vya kihistoria huko Syria na Iraq katika jaribio la "utakaso wa kitamaduni." IS pia limeteka wanawake wengi kama watumwa, hasa kutoka kundi la jamii ya Yazidi. Kundi hilo pia linatumia mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe wa propaganda.
Kwa kiasi gani IS imeiathiri kanda nzima?
Kundi la IS limechochea zaidi mgogoro wa Syria. Mamilioni ya Wasyria na Wairaqi wameyakimbia makaazi yao, wengi wakikimbilia nchi za Ulaya kutafuta hifadhi. Ingawa imepoteza maeneo mengi iliyokuwa ikiyadhibiti, kundi hilo limewacha nyuma uharibifu mkubwa. Maeneo ambayo ilikuwa ikiyadhibiti huenda yakachukua miaka mingi hadi kujengwa tena.