1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lira ya Uturuki yaimarika licha ya onyo la Marekani

17 Agosti 2018

Kauli iliyotolewa na waziri wa fedha ya kusisitiza kuwa mabenki ya nchi hiyo bado ni imara imesaidia kidogo. Pia ahadi iliyotolewa na Qatar ya kuwekeza dola bilioni 15 nchini Uturuki imeibeba sarafu ya Lira.

https://p.dw.com/p/33KFa
Türkische Zentralbank
Picha: Imago/Zuma Press

Sarafu ya Uturuki Lira imepoteza asilimia sita ya thamani yake mbele ya dola ya Marekani wakati ambapo Rais Donald Trump ametishia kuiwekea Uturuki vikwazo zaidi vya kiuchumi ikiwa haitamwachia mchungaji wa Kimarekani Andrew Brunson anaezuwiliwa nchini humo.

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Munichin amesema vikwazo zaidi vya kiuchumi vipo tayari kutekelezwa ikiwa Mchungaji wa Marekani Brunson hataachiwa. Kasisi huyo anakabailiwa na mashtaka ya ugaidi nchini Uturuki.

Wakati huo huo shirika la habari la serikali nchini Uturuki limeripoti kwamba mahakama ya nchi hiyo imeukataa wito wa Marekani wa kutaka mmarekani huyo aachiwe huru. Lakini kuendelea kuwekwa ndani kwa kasisi huyo kunauchochea mvutano uliopo baina ya Uturuki na Marekani na kumechangia katika kuutifua mgogoro wa kifedha unaoikabili Uturuki. Sarafu ya Lira mnamo mwaka huu imepoteza zaidi ya asilimia 40 ya thamani yake mbele ya dola ya Marekani.

Benki ya Uturuki imechukua hatua ili kuiimarisha sarafu ya Lira ikiwa pamoja na kupunguza miamala ya wawekaji vitega uchumi nje ya nchi. Hata hivyo wataalamu wa masuala ya uchumi wamesema Benki kuu ya Uturuki inapaswa kuchukua hatua thabiti za jumla badala ya zile za hapa na pale.

Mchungaji Andrew Brunson mmarekani anayezuiwa nchini Uturuki
Mchungaji Andrew Brunson mmarekani anayezuiwa nchini UturukiPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/E. Tazegul

Gharama za kulipia riba za madeni ya nje zimepanda kwa Uturuki kutokana na thamani ya sarafu  yake ya Lira kupungua. Hata hivyo waziri wa fedha wa Uturuki Berat Albayarak ambae ni mkwe wa rais Erdogan amesema Uturuki itaibuka kutoka kwenye mgogoro huo wa fedha ikiwa imara. Waziri huyo pia amesisitiza kwamba mabenki ya Uturuki yamo katika hali nzuri kabisa. Kauli hiyo inaashiria  kwamba Uturuki itaweza kuhimili vishindo vya Marekani.

Uturuki na kampuni za nchi hizo zinatakiwa kulipa takriban dola bilioni 3.8 kwa ajili ya hatifungani za nje hadi kufikia mwezi wa Oktaba na kwa hivyo gharama ya kulipia riba za madeni zimepanda kwa asilimia 0.25 katika thamani ya Lira. Masoko ya Uturki yanatarajiwa kufungwa jumatatu ijayo kuanzia  mchana kwa ajili ya siku kuu ya Eid ul Adha.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wamesema  pana wasiwasi mkubwa juu ya hali ya uchumi wa Uturuki kwa jumla kutokana na mgogoro wa sarafu yake.  Nchi hiyo inategemea sana bidhaa kutoka nje, kwa karibu mahitaji yake yote ya  nishati  na inalipa kwa fedha za kigeni.

Kwa muda wa miaka mingi Uturuki imekuwa inachukua mikopo katika dola na Lira ili kunufaika na viwango vya riba vya chini. Lakini sasa gharama za kulipia riba hizo zimeongezeka na kwa kampuni zinazoendesha miamala katika msingi wa sarafu ya Lira.

Fedha za Uturuki - Lira
Fedha za Uturuki - LiraPicha: Reuters/M. Sezer

Miongoni mwa nchi zinazoinukia kiuchumi,Uturuki ndiyo yenye deni kubwa kabisa katika fedha za kigeni. Benki ya Societe Generale imekadiria kwamba deni la muda mfupi la nchi hiyo linafikia dola  bilioni 180 na lile la muda mrefu linafikia dola bilioni 460.

Mgogoro wa fedha wa Uturuki kwa jumla umeendelea kuwa mkubwa na mpaka sasa hakuna dalili za kuonyesha iwapo Benki kuu ya nchi hiyo itaruhusiwa kupandisha viwango vya riba ambalo ni suluhisho moja wapo. Kauli iliyotolewa na waziri wa fedha ya kusisitiza kuwa mabenki ya nchi hiyo bado ni imara imesaidia kidogo. Pia ahadi iliyotolewa na Qatar ya kuwekeza dola bilioni 15 nchini Uturuki imeibeba sarafu ya Lira.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/AFPE

Mhariri:  Iddi Ssessanga