Loew atangaza kikosi cha awali cha Ujerumani
16 Mei 2018Kocha wa timu ya Ujerumani Joachim Loew amekitangaza kikosi cha awali cha Kombe la Dunia, ambalo litang'oa nanga Urusi mwezi Ujao. DFB pia imerefusha mkataba wa kocha huyo hadi 2022.
Kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani Joachim Löw amekitangaza kikosi cha wachezaji 27, ambao wataandamana naye kwa ajili ya kambi ya mazoezi nchini Austria wiki ijayo. Hii ina maana kuwa atahitajika kuwapunguza wachezaji wanne kutoka kwa orodha hiyo kabla ya kuelekea Urusi kwa dimba la Kombe la Dunia.
Kando na kuachwa nje kwa kiungo wa Borussia Dortmund Mario Götze, aliyefunga bao la ushindi la Ujerumani katika kombe la dunia nchini Brazil, hakukuwa na majina mengine ya kushangaza kikosini, ambacho kilitangazwa Alhamisi katika jumba la makumbusho ya kandanda la Ujerumani mjini Dortmund. Kuna waliokuwa na maswali ya kama kipa nambari moja Manuel Neuer atachaguliwa, ikizintaiwa kuwa hajacheza mechi yoyote ya ushindani tangu Septemba kutokana na maumivu ya mguu.
Hata hivyo, jina la Neuer lipo kwenye orodha hiyo, mmoja wa makipa wanne watakaosafiri kwenda Austria. Löw amesema Neuer atayanoa makali kwa kucheza katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu ya Ujerumani ya wachezaji wa chini ya miaka 20 katika kipindi hiki cha maandalizi.
Kikosi cha awali cha Ujerumani:
Walinda mlango: Bernd Leno (Bayer Leverkusen), Marc-Andre ter Stegen
(Barcelona), Kevin Trapp (Paris Saint-Germain), Manuel Neuer (Bayern
Munich)
Mabeki: Jerome Boateng (Bayern Munich), Matthias Ginter (Borussia
Moenchengladbach), Jonas Hector (Cologne), Mats Hummels (Bayern
Munich), Joshua Kimmich (Bayern Munich), Marvin Plattenhardt (Hertha
Berlin), Antonio Ruediger (Chelsea), Niklas Suele (Bayern Munich),
Jonathan Tah (Bayer Leverkusen)
Viungo: Julian Brandt (Bayer Leverkusen), Julian Draxler (Paris
Saint-Germain), Leon Goretzka (Schalke), Ilkay Guendogan (Manchester
City), Sami Khedira (Juventus), Toni Kroos (Real Madrid), Thomas
Mueller (Bayern Munich), Mesut Oezil (Arsenal), Sebastian Rudy
(Bayern Munich), Leroy Sane (Manchester City), Marco Reus (Borussia
Dortmund)
Washambuliaji: Timo Werner (Leipzig), Mario Gomez (Stuttgart), Nils
Petersen (Freiburg)
Mkataba wa Loew umerefushwa
Hatua ya kuurefusha mkataba wa Löw sio ya kushangaza kwa sababu Rais wa Shirikisho la Kandanda Ujerumani – DFB Reinhard Grindel alikuwa amesema awali kuwa kocha huyo ataendelea kuiongoza timu ya taifa, hata kama Ujerumani itaondolewa katika robo fainali ya Kombe la Dunia la Urusi. Mikataba ya kocha msaidizi Thomas Schneider na mwalimu wa makipa Andreas Köpke pia imerefushwa hadi 2022.
Mkataba wa mkurugenzi wa DFB na meneja mkuu wa timu ya taufa Oliver Bierhoff imerefushwa hadi 2024.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Sekione Kitojo