Lukas Podolski kurejea FC Cologne ?
12 Novemba 2008Msimu wa sherehe za kanivali ulianza juzi tarehe 11.11. mjini Cologne,mojawapo ya mashina ya sherehe hizo za kila mwaka.Mashabiki wa FC Cologne ilioanza kutamba kama zamani katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, wangependa sana kilele cha sherehe zao hizo kiwe kurejea kwa mwanamfalme wao wa dimba "Prince Lukas podolski" aliehamia Bayern Munich.Mashabiki wengi wa kanivali juzi walivaa jazi No.20-jazi aliowaachia Lukas Podolski kabla kuhamia Bayern munich ambako kwa sasa haridhiki.
Stadi mwengine wa zamani wa FC Cologne,Bernd Schuster, kocha wa Real Madrid ya Spain, huenda akatimuliwa,kwani Real imekiona kilichomtoa kanga manyoya juzi ilipotolewa nje ya kombe la Spain na timu ya daraja ya tatu.
Stadi wa Werder Bremen kutoka Peru, Claudio Pizarro amepigwa faini ya dala 3.800 kwa kumbughudhi rifu.
Soga la Lukas Podolski anaetamba akiichezea timu ya taifa,lakini kwa mabingwa Bayern Munich haishi kuwekwa ubaoni kama mchezaji wa akiba,haliishi.Swali linaloulizwa :Je, atarudi Cologne Januari mwakani ? Mada hii haizungumzwi tu katika sherehe hizo za kanivali zinazoendelea hadi Februari 25 zitakyapofikia kilele chake kandoni mwa mto Rhein,bali hata mkoani Bavaria,nyumbani mwa mabingwa Bayern Munich. Podolski,mzaliwa wa poland,aliekulia na FC Cologne, hafichi na kuweka siri mapenzi yake kwa Fc Cologne-klabu aliyojiunga nayo akiwa na umri wa miaka 10 1995 na hata kuwa nahodha wake baadae.Aliichezea Cologne katika daraja ya pili ya Bundeliga akiwa pia mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani.
podolski alijiunga na B.munich 2006,lakini kinyume na alivyokua Cologne,hakutamba,kwani Munich ina mastadi wengi kama podolski-akina Luca Toni wa Itali,Robbery wa Ufaransa,Ze Roberto wa Brazil na Miroslav klose wa Ujerumani.
Wote hao wamemfunika Podolski asionekane,wakati akiichezea Cologne , yeye ni nyota pekee inayonawiri mawinguni.
Podolski ametia mabao 31 katika mechi 59 alizoichezea timu ya taifa.
Akionesha hasira ,meneja wa Bayern Munich Uli Hoenes-maarufu kwa ulimi wake mkali alisema, "Kwa podolski kuna Cologne pekee,kila mara Cologne,Cologne,Cologne."Anaiota Cologne usiku na mchana.Hoeness wiki hii alikanusha ripoti ya jarida la dimba Kicker kuwa halmashauri kuu ya B.munich imeridhia kumuachia Podolski kuihama Munich hapo januari mwakani ingawa mkataba wake na b.Munich unadumu hadi 2010.Kima cha Euro milioni 10 kimetajwa kumkomboa Podolski kima sawa na kile Munich ililipa kumnunua podolski miaka 2 iliopita kutoka FC Cologne.
Mtiaji mabao hatari wa Werder Bremen katika Bundesliga, Claudio Pizarro amepigwa faini ya dala 3.800 na shirikisho la dimba la Ujerumani. Kisa ni kuwa pizarro alitoa maneno ya kumkashifu rifu mwishoni mwa wiki wakati wa mpambano na Buchum. Alinukuliwa kusema,
"Tunacheza dhidi ya wachezaji 12 kutoka Bochum.Rifu alichezesha vibaya sana." Alisema hayo Pizarro baada ya Bremen kumudu suluhu tu na Bochum ya 0:0 jumamosi iliopita.
Bernd Schuster,mjerumani na kocha wa mabingwa mara kadhaa wa ulaya Real Madrid, ameonywa ama Real ama inatamba jumamosi hii mbele ya Villareal au afunge virago.Magazeti ya spoti ya jiji la Madrid- AS na Marca yaliarifu kwamba Real imepoteza imani na kocha huyu mbishi wa kijerumani baada ya Real Madrid kuchezeshwa kindumbwe-ndumbwe na timu ya daraja ya 3 ya Spian -Union Irun na kutolewa katika kombe la taifa. Schuster aliwakera mashabiki wa Real kwa kuteremsha timu ya wachezaji wa akiba akitumai wangetosha kutamba mbele ya chipukizi hao.
Spain licha ya misukosuko ya mabingwa wao Real Madrid,kama mabingwa wa Ulaya wangali kileleni mwa orodha ya timu bora za dunia za FIFA iliotoka jana.Uingereza imechupa nafasi 4 na kujiunga na timu 10 bora ulimwenguni.Spian inaongoza nambari one ikifuatwa na Ujerumani huku mabingwa wa dunia Itali wakiangukia nafasi ya tatu.Holland iko nafasi ya 4 mbele ya Brazil inayoiacha Argentina nafasi ya 6.
Timu zilizopiga hatua katika orodha iliotoka ni Jamaica, walioondoka nafasi ya 116 na kufikia ya 83 baada ya kutamba katika kinyanganyiro cha kuania tiketi ya kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika kusini, dhidi ya Mexico na Hondurus.Switzerland chini ya kocha wao Ottmar Hitzfeld wamechupa nafasi 18 hadi ya 27.