1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa ya kibinadamu Pakistan

26 Mei 2009

Majeshi ya Pakistan yakijongelea ngóme za wapiganaji wa Taliban katika Bonde la Swat,shirika la Human Rights Watch linalotetea haki za binadamu limeonya juu ya maafa ya kibinadamu.

https://p.dw.com/p/HxaU
Pakistan army soldiers patrol on a road to Pakistan's troubled Swat valley, where security forces are fighting with Taliban militants, at Dargai, 90 kilometers (56 miles) from Peshawar, Pakistan on Friday, May 8, 2009. Pakistani jets screamed over a Taliban-controlled town Friday and bombed suspected militant positions as hundreds of thousands fled in terror and other trapped residents appealed for a pause in the fighting so they could escape.(AP Photo/Mohammad Sajjad
Wanajeshi wa Pakistan wakipiga doria katika Bonde la Swat wanakopigana na wanamgambo wa Taliban.Picha: AP

Operesheni ya majeshi dhidi ya wanamgambo wa Taliban ikiendelea kwa juma la tano, maafisa wa usalama wanasema vikosi vya serikali vimedhibiti asilimia 70 ya mji mkuu wa Bonde la Swat Mingora. Vikosi hivyo vimejiimarisha na vinasaka nyumba moja moja katika eneo hilo. Wakati huo huo ripoti zinasema ndege za kijeshi leo zimeshambulia pia vituo vya Taliban katika Wilaya ya Waziristan ya Kusini.

Operesheni ya kijeshi ikiendelea, wafanyakazi wa Human Rights Watch wanasema uhaba wa chakula, maji na dawa unasababisha maafa makubwa ya kibinadamu kwa wakazi walionasa katika eneo hilo kwa sababu ya amri inayowazuia kutoka nje. Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika kanda ya Bara la Asia, Brad Adams amesema, serikali haiwezi kuwazuia wakaazi hao bila ya kuwakidhia mahitaji yao muhimu. Mapigano katika Bonde la Swat yamesababisha hadi watu milioni 2.3 kukimbia makwao, lakini kama watu 200,000 wamenasa katika eneo hilo la mapigano makali. Kwa mujibu wa mratibu wa misaada ya serikali ya Pakistan, Luteni Jenerali Nadeem Ahmed, ndege huenda zikadondosha vyakula kwa ajili ya raia walionasa. Amesema, raia hao wameshauriwa kubakia kule waliko kwa sababu ya usalama wao, badala ya kusafiri katika maeneo ya mapigano ndani na ukingoni mwa mji mkuu Mingora.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa unazingatia kuliomba jeshi la Pakistan kusitisha mapigano yake kwa muda, ili raia walionasa waweze kupatiwa msaada wa dharura. Kwa maoni ya Human Rights Watch, jeshi la Pakistan lazima lichukue hatua za kuwasaidia wakaazi wanaoteseka katika Bonde la Swat badala ya kuongeza shida zao, ikiwa serikali inataka kuwashinda wapiganaji wa Taliban. Ripoti mbali mbali kutoka eneo hilo zinasema, raia ni wahanga wa ukatili unofanywa na wanamgambo wa Taliban na vile vile mashambulio ya jeshi. Mjini Mingora,raia mmoja aliekataa kutaja jina lake amesema kuwa hadi kama siku nne za nyuma, wanamgambo wa Taliban waliopania kutumia sheria za Kiislamu, walikuwa wakipiga doria mitaani, lakini sasa maiti zao zimeenea njiani.

Serikali ya Pakistan ilianzisha operesheni hiyo dhidi ya Taliban mapema mwezi huu baada ya waasi hao kukiuka makubaliano ya amani katika Bonde la Swat na kuendelea kuteka maeneo ya jirani na kusonga mbele hadi kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Pakistan Islamabad.

Mwandishi: P.Martin

Mhariri: Abdul-Rahman