1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya COVID-19 duniani yapindukia milioni 400

Sylvia Mwehozi
9 Februari 2022

Visa vya maambukizi ya Covid-19 ulimwenguni kote vimepindukia milioni 400, kulingana na takwimu za shirika la habari la Reuters huku kirusi cha Omicron kikichangia kwa kiasi kikubwa idadi hiyo.

https://p.dw.com/p/46l4g
Russland Sankt Petersburg Krankenhaus Covid
Picha: Valentin Yegorshin/TASS/dpa/picture alliance

Kirusi cha Omicron ambacho ndio kimetawala ongezeko la maambukizi ulimwnguni kote, kimechangia karibu visa vyote vipya vinavyoripotiwa kila siku. Zaidi ya visa milioni mbili bado vinaripotiwa angalau kwa wastani kila siku kulingana na takwimu za Reuters. Vifo navyo vimeongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi wiki tano zilizopita kwa kuzingatia maambukizi ya siku saba.

Wakati ushahidi wa awali katika baadhi ya nchi ukionyesha kuwa kirusi cha Omicron hakina makali ukilinganisha na aina nyingine zilizopita, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba idadi kubwa ya maambukizi inaweza kuelemea mifumo ya afya kote duniani.

Nchi zinazoongoza kuwa na maambukizi makubwa ni Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Brazil. Marekani inaongoza kwa maambukizi ya kila siku huku visa milioni moja huripotiwa kila baada ya siku tatu.

Karibu nusu ya maambukizo yote mapya ulimwenguni kote yameripotiwa barani Ulaya huku jumla ya nchi 21 zikiwa bado katika wimbi la maambukizi. Hata hivyo baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza taratibu kuondoa vizuizi. Uhispania, imefutilia mbali sharti la watu kuvaa barakoa wanapokua nje kuanzia kesho Alhamis. 

Russland Sankt Petersburg Krankenhaus Covid
Hali ya Covid-19 nchini UrusiPicha: Valentin Yegorshin/TASS/dpa/picture alliance

Kuanzia siku ya Jumatatu Ugiriki iliruhusu watalii waliopata chanjo Ulaya kuingia nchini humo. Ijumaa iliyopita idadi ya vifo nchini India ilipindukia 500,000 huku wataalamu wa afya wakisema kwamba kiwango hicho kilikiukwa mwaka jana kutokana na takwimu kutokuwa sahihi na vifo ambavyo havikuhesabiwa.

Wakati huohuo shirika la Kudhibiti Madawa barani Ulaya, EMA limesema linaanza kutathmini chanjo za nyongeza za BioNTech-Pfizer kwa watoto wenye kati ya umri wa miaka 12 na 15. Wiki iliyopita, EMA ilisema itatoa uamuzi hivi karibuni juu ya ombi kama hilo la kuwapa chanjo ya nyongeza vijana wenye umri wa miaka 16 na 17.

EMA imesema ombi la vijana wenye umri wa miaka 16 na 17 bado linaendelea. Kwengineko, wanasayansi wa China wamesema wametengeneza vipimo vya COVID-19 ambavyo vinatoa majibu ndani ya dakika nne. Vipimo hivyo vina uhakika kama vipimo vya PCR vinavyofanywa maabara. Nalo Shirika la Afya Duniani, WHO limesema leo kuwa linahitaji dola nyingine bilioni 16 kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini kupambana na janga la virusi vya corona.