1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya ini kwa watoto yaiumiza kichwa WHO

3 Mei 2022

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limearifu kuhusu visa 228 vinavyohisiwa kuwa ni maambukizi ya homa ya ini kwa watoto ambayo hata hivyo bado hayajajulikana chanzo chake.

https://p.dw.com/p/4Alds
Symbolbild I Hepatitis A Virus
Picha: IMAGE POINT FR/LPN/picture alliance

Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hadi Mei 1, takriban visa 228 vilikuwa vimeripotiwa kwenye shirika hilo kutoka mataifa hayo 20, na visa vingine 50 bado vinachunguzwa. Amesema visa vingi miongoni mwa hivyo vimeripotiwa kutoka Ulaya, lakini kuna vingine viliripotiwa kutoka Marekani, mashariki mwa Pasifiki na Kusinimashariki mwa Asia.

Scotland ilikuwa ya kwanza kuliarifu shirika hilo juu ya visa 10 vilivyogunduliwa kwa watoto wa chini ya miaka 10, lakini hadi sasa visa 100 vimerekodiwa nchini Uingereza. Baadhi ya visa hivyo vimesababisha ini kushindwa kufanya kazi vizuri na kwa maana hiyo wagonjwa walitakiwa kupandikizwa ini jipya. Hadi sasa mtoto mmoja amekwishafariki dunia kutokana na maambukizi hayo.

Deutschland Eberswalde | Säugling Spritze | Impfschutz
Mtoto mdogo akichomwa chanjo ya kumkinga na maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maambukizi ya ini.Picha: Hans Wiedl/dpa/picture alliance

Shirika hilo linarejelea mlipuko mkali wa kuvimba ini kama homa kali ya ini kwa watoto wadogo ambayo chimbuko lake bado halijajulikana.

Hata hivyo limethibitisha kuhusu kuendelea na uchunguzi wa chimbuko la maambukizi hayo, wakati likiwa linavuchunguza virusi vya Adeno "Adenoviruses" ambavyo hujulikana zaidi kwa kusababisha dalili za maradhi katika njia ya upumuaji, kwenye macho na hata kusababisha matatizo kwenye mmeng'enyo wa chakula.

WHO limesema virusi vya kawaida vinavyoweza kusababisha maambukizi makali ya homa ya ini (Hepatitis A,B,C,D na E) havikuonekana katika kisa hata kimoja, miongoni mwa visa vya awali 169 vilivyochunguzwa.

Mashirika: AFPE