Maambukizi ya virusi vya Corona Afrika yaongezeka
20 Machi 2020Nigeria imesema inafunga mashule yote nchini humo na kupunguza shughuli za mikutano ya kidini katika mji wa biashara wa Lagos na mji mkuu Abuja, wakati Afrika kusini , nchi ambayo ina uchumi mkubwa wa viwanda barani humo, imechukua hatua ya kupunguza riba kusaidia makampuni nchini humo.
Nigeria, nchi ambayo ina wakaazi wengi zaidi katika bara la Afrika na ambayo ina wakaazi wanaofikia milioni 200, hadi sasa imerekodi idadi ya watu 12 walioambukizwa virusi vya Corona na unafuatia nchi nyingine katika kuongeza hatua zake za kupambana na virusi hivyo. Serikali ya jimbo la Lagos imesema shule katika mji huo ambao una wakaazi wapatao milioni 20 zitafungwa kuanzia siku ya Jumatatu. Serikali ya mji huo imesema kwamba sasa kuna maambukizi yanayotoka ndani ya mji huo.
Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Afrika kusini sasa imepindukia watu 200 leo Ijumaa wakati waziri wa afya Zweli Mkhize akionya kuwa nchi hiyo bado imo katika njia ndefu katika mapambano yake dhidi ya ugonjwa huo.
Na katika hatari ya maambukizi kutokea ndani ya Afrika kusini , nchi hiyo imesema maambukizi kwa watu watano kati ya maambukizi mapya ni watu waliohudhuria ibada katika kanisani linalochukua zaidi ya watu 200 katika jimbo la kati la Free State. Maafisa wanachukua hatua za haraka kuwapata watu wengine waliohudhuria ibada hiyo.
Mfanyakazi wa hospitali aambukizwa
Kesi nyingine mpya nchini Afrika kusini ya maambukizi ni mfanyakazi wa hospitali ambaye amekuwa katika hospitali kadhaa za binafsi nchini humo.
Mamlaka ya bandari nchini Afrika kusini nayo imesema kwamba uchunguzi umeonesha kuwa watu waliokuwa katika meli ya kitalii pamoja na meli ya mizigo hawana virusi vya Corona , baada ya watu hao kuwekwa katika karantini nje ya bandari ya Cape Town kutokana na shaka ya kuzuka virusi vya Corona.
Hali ya hatari ya kiafya itawekwa nchini Morocco leo, wakati serikali ikilenga katika kupunguza nyendo za watu ili kuzuwia kusambaa kwa virusi vya Corona. Hatua hizo ambazo ni maalum, zitaanza rasmi usiku wa leo nchini humo, imesema wizara ya mambo ya ndani.
Ni wafanyakazi wa sekta maalum tu ndio watakaoruhusiwa kutembea na kwenda makazini, kama wafanyakazi wa hospitali na mabenki pamoja na wale ambao wanafanyakazi katika vituo vya kuuzia mafuta pamoja na huduma za chakula na wale wanaotoa huduma muhimu , shirika la habari la Morocco limenukuu duru za wizara hiyo zikisema jana.
Nayo Niger imekuwa nchi ya 36 barani Afrika kuthibitisha kuwa na mgonjwa wa COVID 19. Mtu huyo anayefanyakazi katika kampuni ya usafirishaji amekuwa mgonjwa wa kwanza katika taifa hilo la Afrika magharibi .