Maambukizi ya virusi vya corona yafikia milioni moja
3 Aprili 2020Kufikia leo Ijumaa ugonjwa huo umewakumba zaidi ya watu milioni moja duniani kote. Na watu milioni 10 wamepoteza ajira nchini Marekani kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Mzozo wa kiafya unaongezeka mjini New York , ambako kampuni moja ya mazishi katika eneo ambalo limeathirika zaidi , lilikuwa na miili 185 iliyolundikana , zaidi ya mara tatu ya uwezo wake wa kawaida. Mji huo umeshuhudia takriban vifo 1,500 kutokana na virusi hivyo.
Duniani kote idadi ya maambukizi yaliyoripotiwa imefikia katika hali ya kutisha ya watu milioni moja, ambapo watu 53,000 wamefariki, kwa mujibu wa data kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Lakini idadi halisi inaaminika kuwa juu zaidi kwasababu ya ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, wakati kesi ndogo ndogo nyingi haziripotiwi, na nchi kadhaa zinaficha kiwango cha maambukizi.
Uhispania jana iliripoti idadi ya juu kabisa ya vifo kwa siku, ambapo watu 950 walifariki, na kufikisha idadi ya jumla ya watu waliofariki kufikia 10,000, licha ya ishara kuwa kiwango cha maambukizi kinapungua. Italia imerekodi vifo 760, na kufikisha idadi ya vifo 13,900, ikiwa ni hali mbaya kabisa kuliko nchi yoyote, lakini maambukizi mapya yanaendelea kupungua pia.
Idadi ya vifo yaongezeka
Ufaransa imerekodi jumla ya vifo 4,500 katika hospitali, ambapo vifo 471 ni katika siku moja iliyopita. Lakini maafisa wanatarajia idadi jumla ya vifo kuchupa kwa kiasi kikubwa kwasababu ndio kwanza wanaanza kuhesabu vifo katika majumba ya kuwahifadhi wazee pamoja na maeneo mengine kwa ajili ya wazee.
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa jana liliidhinisha azimio linalotoa wito wa ushirikiano wa kimataifa pamoja na juhudi za pamoja katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19, katika waraka wa kwanza kutolewa na chombo hicho cha kimataifa tangu kuzuka kwa ugionwa huo.
Azimio hilo lililoidhinishwa kwa kauli moja , pia linasisitiza, "haja ya kuheshimu haki za binadamu" na kwamba "kuna nafasi kwa aina yoyote ya ubaguzi, na chuki dhidi ya wageni katika kupambana na janga hili."
Urusi ilishindwa katika juhudi zake za kupinga azimio hilo kwa kutoa mswada wake binafsi kwa maelezo kwamba umeungwa mkono na mataifa manne.
Mashirika ya ndege ulimwenguni yamepoteza kiasi ya asilimia 80 uwezo wa kubeba abiria kimataifa ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita na nusu ya ndege duniani zimeegeshwa, data mpya zinaonesha, zikieleza kuwa sekta hiyo ya safari za anga huenda ikachukua miaka kurejea katika hali ya kawaida kutokana na janga la virusi vya corona.