1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya virusi vya Corona yazidi kwenye nchi kadhaa

Zainab Aziz Mhariri:Sylvia Mwehozi
23 Februari 2020

Wizara ya afya ya Iran imefahamisha juu ya kuongezeka idadi ya vifo kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona. Hadi kufikia Jumapili wasiwasi huo umeongezaka pia katika nchi za Italia na Korea Kusini

https://p.dw.com/p/3YEqn
Ausbreitung der Coronavirus in Iran
Picha: titrebartar

Msemaji wa wizara ya afya ya Iran Kianoush Jahanpour amesema watu zaidi ya 42 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo nchini Iran na kutoka Jumamosi jumla ya watu sita walifariki. Mlipuko wa homa inayosababishwa na virusi vya Corona nchini Iran ulianzia kwenye mji wa Qom, lakini umeenea haraka katika siku chache zilizopita katika miji mingine minne ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Tehran.

Nchini Italia idadi ya watu walioambukizwa pia imeongezeka hasa katika mji wa Lombardy, ulio kwenye mkoa wa kaskazini mwa Italy. Mji mkuu wa masuala ya uchumi nchini Italia, Milan upo katika mkoa huo.

Mamlaka nchini Italia imetangaza marufuku ya kufanyika hafla za za sherehe za Carnival katika juhudi za kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona, huku idadi ya watu walioambukizwa nchini humo ikiwa imefikia watu 133 kufikia siku ya Jumapili. Mkuu wa mkoa wa Veneto Luca Zaia amesema marufuku hiyo itaanza Jumapili jioni. Sherehe hizo za Carnival, ambazo huwakutanisha maelfu ya watu zingeliaendelea hadi siku ya Jumanne wiki ijayo.

Kiongozi wa Iran Ali Khamenei
Kiongozi wa Iran Ali KhameneiPicha: picture-alliance/AA/Iranian Supreme Leader Press

Mamlaka ya mji wa Venice imesema watu watatu katika mji huo wameambukizwa virusi hivyo na wote ni wazee walio na miaka 80 na zaidi na wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi.

Korea Kusini imeendelea na kuweka hali tahadhari kwa kiwango cha juu kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi ya homa ya corona. Rais Moon Jae-in amesema nchi yake imechukua hatua hiyo baada ya idadi ya maambukizi kupanda karibu mara tatu zaidi kufikia mwishoni mwa wiki hadi zaidi ya maambukizi 600.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) pia lilitahadharisha mifumo mibaya ya kiafya ya Kiafrika iliiachilia hatari ya ugonjwa wa COVID-19, ambao sasa umevuka mipaka ya China na kuenea katika nchi zaidi ya 25.

Mgonjwa wa Corona anaandaliwa kupelekwa hospital nchini Italia
Mgonjwa wa Corona anaandaliwa kupelekwa hospital nchini ItaliaPicha: picture-alliance/Photoshot

Mikoa ya Kusini ya nchi za Uswisi na Austria inachukua hatua za kuzuia kusambaa kwa maambukizi kutoka nchi jirani ya Italia. Jimbo la Ticino nchini Uswizi limetangaza kwamba hospitali zake zitawafanyia vipimo watu wote wenye dalili za aina ya ugonjwa wa Covid-19, hata ikiwa hawana uhusiano wowote na China au na watu wengine walioambukizwa.

Ticino ni mkoa unaopakana na mkoa wa Lombardia ulio na watu walioathirika na virusi Corona nchini Italia. Takriban watu 68,000 husafiri kutoka Italia kwenda Ticino kwa ajili ya kufanya kazi kila siku. Gavana Peter Kaiser wa jimbo la Carinthia nchini Austria, amewaambia watu wajizuie kusafiri kwenda kwenye maeneo yaliyoathiriwa na virusi vya corona nchini Italia.

Vyanzo:/AP/AFP/DPA