Maandalizi ya kabla ya kuanza Bundesliga
10 Julai 2017Klabu ya mwisho kujiunga na vilabu vingine katika maandalizi hayo ni Borussia Dortmund ambayo ilifanya hivyo tarehe 7 Ijumaa mwezi huu, wakati vilabu vingine tayari vilianza mchakato huo katikati ya mwezi uliopita.
Mbali na maandalizi hayo pia kuna heka heka ya nani anajiunga na timu gani na nani anahamia kwingine. Kwa kuwa dirisha la usajili halijafungwa hadi mwezi wa nane , bado kuna tetesi za hapa na pale za wachezaji kuzihama timu zao kutafuta malisho bora zaidi na pia kutafuta maeneo ya kujulikana na kuongeza kiwango chao zaidi.
Antonio Rudiger mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani na bingwa wa kombe la mabara, Confed Cup, anahamia Chelsea katika ligi ya England ambapo inasemekana kocha mkuu wa timu hiyo Antonio Conte anapanga msimu ujao kuichezesha timu yake kwa mfumo wa 3-4-3, ambapo ulinzi wa timu hiyo utakuwa na wachezaji watatu pamoja na David Luiz, Gary Cahill na Antonio Rudiger.
Mfumo huo ulitumika sana msimu uliopita na timu za Ujerumani, kama vile 1899 Hoffenheim na ukaifikisha timu hiyo kucheza ligi ya mabingwa Ulaya , Champions league msimu ujao, Schalke 04, na mahasimu wao wakubwa Borussia Dortmund ambao walitumia mtindo huo mara chache wanapoona kuna ulazima.
Anthony Modeste mwenye umri wa miaka 29 na ambaye msimu uliopita alichuana vikali na wakali kama Robert Lewandowski (Bayern Munich)na bingwa wa mtutu wa bunduki Pierre Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund katika kuwania mtutu huo, alifanikiwa kupachika mabao 25 kwa FC Kolon na kuisaidia timu hiyo kufikia kucheza ligi ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka zaidi ya 25,lakini ameamua kuipa kisogo timu hiyo na kwenda katika klabu ya Tianjian Quanjian ya China.
Pia ligi ya Ujerumani itamkosa Philipp Lahm , Xabi Alonso ambao wametundika madaluga yao, Douglas Costa wote wa Bayern Munich anahamia Juventus Turin kwa mkopo licha ya kwamba mazungumzo kuhusu uhamisho bado yanaendelea.
Ligi inaanza tarehe 18 Agosti.
Marefa wa Ujerumani wako tayari kwa ajili ya kutumia mfumo wa video wa kuangalia makosa ya refa katika msimu ujao na hawata tumbukia katika utata na uchelewesho ulijitokeza hivi karibuni katika michezo ya Confed Cup , amesema mwamuzi mmoja Hellmut Krug leo. Krug aliliambia toleo la gazeti la michezo la Ujerumani Kicker kwamba marefa wote wa vodeo wamehusika na majaribio kadhaa ya mtandaoni na nje ya mtandao , na pia kama marefa wanaoongoza mchezo.
Krug ambaye anaongoza kitengo cha mradi wa marefa wa video (VAR) nchini Ujerumani , amesema uamuzi bila shaka hautachukua muda mrefu kama ilivyotokea katika kombe la dunia la vijana chini ya umri wa miaka 21 na kombe la mabara Cofed Cup.
VAR itafanyiwa majaribio rasmi katika msimu huu wa Bundesliga ,ambao shirikisho la soka duniani FIFA litaamua Machi mwakani iwapo mfumo huo utumike rasmi.
Na katika ligi ya England Romelu Lukaku ameiaga rasmi FC Everton wakati akitafakari maisha yake akiwa na Manchester United , baada ya kukamilisha uhamisho wa pauni milioni 75, sawa na Euro milioni 85.5.
Pia Klabu ya Premier League ya England ya Tottenham Hotspurs imesema haiko katika mazungumzo ya kununuliwa baada ya kuzuka taarifa katika vyombo vya habari vya England kwamba mnunuzi ambaye anasaidiwa na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Facebook Mark Zuckerberg anatafakari kutoa kiasi cha pauni bilioni 1, dola bilioni 1.29 kuinunua klabu hiyo.
Gazeti la Sunday Times liliripoti jana kwamba kampuni ya uwekezaji ya Marekani Iconiq Capital imefanya mazungumzo na kampuni kadhaa zinazotaka kununua juu ya uwezekano wa kuinunua klabu hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / ZR
Mhariri: Josephat Charo