1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa: Maandamano kupinga sheria ya usalama wa taifa

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
31 Januari 2021

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika miji kadhaa nchini Ufaransa kupinga muswada wa usalama ambao wanasema utawazuia watu kurekodi na kuchapisha video zinazohusiana na ukatili wa polisi.

https://p.dw.com/p/3ocqC
Frankreich Protest "Global Security Bill' in Paris
Picha: Bennoit Tessier/REUTERS

Kulingana na waandaaji wa maandamano hayo, kulikuwa na mikusanyiko zaidi ya 55. Wanaharakati wa vuguvugu la Fulana za Manjano lililoshika kasi kwa zaidi ya mwaka mmoja nchini Ufaransa pia walishiriki kwenye maandamano hayo.

Kutokana na maandamano ya mara kwa mara, kifungu chenye utata cha 24 kulingana na sheria ya usalama wa taifa kitafanyiwa marekebisho ambapo waandamanaji hao wanapinga rasimu ya sheria hiyo ambayo itazuia shughuli za upigaji picha au kuwarekodi polisi. Raia wa Ufaransa pia wanapinga utumiaji wa zana za ufuatiliaji kama ndege zisizo na rubani na kamera zinazowafuatilia watembea kwa miguu.

Wanaharakati wanataka kifungu hicho cha 24 kifutwe kabisa lakini chama kinachotawala cha LREM cha Rais Emmanuel Macron kinakusudia kuipitisha sheria hiyo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Yoan Valat/AP Photo/Yoan Valat

Video iliyosambazwa ikiwaonesha polisi wazungu wakimpiga mtayarishaji wa muziki mweusi katika studio yake ya mjini Paris mnamo Novemba 21 ni tukio lililochochea hasira za watu juu ya sheria hiyo mpya, inayopingwa na wengi wanaosema inaashiria kuwa rais Macron anageukia siasa za mrengo wa kulia. 

Serikai ya Ufaransa yasemaje

Serikali ya Ufaransa imesema sheria iliyopendekezwa inahitajika kwa sababu maafisa wa polisi wamekuwa ni walengwa, wanashambuliwa na miito ya vurugu dhidi yao imeongezeka kwenye mitandao ya kijamii. Serikali imesema sheria hiyo itawalinda vyema polisi.

Kwa upande wake vyombo vya habari nchini Ufaransa vinasema mpango huo wa utekelezaji wa sheria hiyo mpya ya usalama wa taifa unatumiwa kuvizuia vyombo vya habari kutangaza juu ya maandamano ya kupinga serikali.

Sheria hiyo ambayo tayari imeidhinishwa na bunge, itapelekwa kwenye baraza la Seneti, ambalo ni tawi la juu la bunge la Ufaransa, mnamo mwezi Machi.

Mnamo mwezi Januari, maelfu ya watu waliandamana kupinga sheria hiyo katika mji mkuu wa Paris na katikamiji mingine kote nchini Ufaransa.

Vyanzo:AFP/DPA