Maandamano mapya yaitishwa leo Misri
23 Agosti 2013Kundi hilo lililoongoza maadamano dhidi ya utawala wa Rais Hosni Mubarak lijulikanalo kama Vuguvugu la Aprili 6, limesema hatua ya kumwachia huru kiongozi huyo kutoka gerezani, inalenga kupotosha mkondo wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani, Februari mwaka 2011.
Mahakama nchini Misri jana iliamua Mubarak aachiwe kutoka gerezani, na hivi sasa amewekwa katika kizuizi cha nyumbani.
Wakati Vuguvugu hilo likipanga kuandamana kupinga kuachiwa kwa Mubarak, makundi ya wanaharakati wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Mursi, nao wameandaa maandamano makubwa kulipinga jeshi hilo, katika kile kinachochukuliwa kama kuupima uwezo wanaobaki nao kuweza kuhamasisha uungwaji mkono, wiki saba baada ya kuangushwa kiongozi wao.
Wengi hawana hamu kurudi mitaani
Viongozi wengi wakuu wa makundi hayo wamekamatwa siku za hivi karibuni, hali ambayo imeathiri uwezo wao wa kukusanya wafuasi, na kuzusha maswali juu ya nguvu yaliyobaki nayo makundi hayo yanayojiita Muungano dhidi ya Mapinduzi ya Kijeshi.
Ukandamizaji ulioambatana na umwagaji damu mkubwa dhidi ya makundi haya umeifanya idadi ya watu wanaoitikia maandamano kupungua sana. Mmoja wa viongozi wa kundi la Udugu wa Kiislamu ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kwa sasa mawasiliano kwa njia ya simu yamesimamishwa, na viongozi wengi wa Udugu wa Kiislamu hivi sasa wako mafichoni, kwa hofu ya kukamatwa.
Mtu huyo alisema kuwa wafuasi wa kundi hilo kwa sasa hawawezi kupata maelekezo yoyote kutoka kwa viongozi wao, na hawajui cha kufanya.
Viongozi wa Udugu wa Kiislamu ambao wamewekwa kizuizini ni pamoja na Mohamed Mursi mwenyewe ambaye anazuiliwa mahali pasipojulikana, na kiongozi wa kiroho wa kundi hilo, Mohamed Badie, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa kiitikadi kutiwa mbaroni tangu mwaka 1981.
Mubarak nje, Mursi ndani
Kubakia gerezani kwa viongozi hao wakati ambapo Mubarak ameachiwa, licha ya ukweli kuwa hata yeye anatuhumiwa kwa mauaji ya waandamanaji, kumezusha mjadala mkubwa.
Hata hivyo, si wanaharakati wengi wanaojisikia tayari kuandamana tena mitaani, kutokana na hofu ya ghasia za hivi karibuni nchini humo.
Bado Mubarak anakabiliwa na mashitaka mengine na atafikishwa tena mahakamani Jumapili ijayo, siku ambayo pia Bedie na viongozi wengine wa Udugu wa Kiislamu watasimamishwa kizimbani.
Marekani imejitenga mbali na hatua ya kuachiwa kwa Mubarak kutoka gerezani, ikisema huo ni uamuzi wa Wamisri wenyewe. Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo, Jen Psaki, alisema msimamo wa Marekani kuhusu Mursi unabakia pale pale, kwamba lazima uwepo utaratibu wa kumuachia huru kutoka kizuizini.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef