Maandamano ya kupinga serikali Iran yamemalizika
3 Januari 2018Matamshi hayo ni ya kwanza ya uungaji mkono kutoka kwa viongozi wa kanda hiyo. Wakati huo huo ujerumani imesema .inafuatia yale yanayotokea nchini Iran ikiwa na wasi wasi , lakini imesisitiza kwamba waandamanaji wanaoandamana kupinga ughali wa maisha wanapaswa kuheshimiwa.
Chanzo katika ofisi ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kimesema rais alijadili machafuko ya wiki nzima nchini Iran wakati akizungumza na rais Rouhani kwa simu. Rais wa Iran alimwambia Erdogan ana matumaini maandamano yatamalizika katika siku chache ", chanzo hicho kimesema.
Mamia ya Wairan walishiriki katika maandamano ya kuiunga mkono serikali katika miji kadhaa leo katika kile kinachoelezwa kuwa ni tukio lililotayarishwa na serikali kuonesha nguvu zake baada ya siku sita za machafuko mitaani ambayo yameutikisa uongozi wa kidini na kusababisha watu 21 kuuwawa.
Haki ya kuandamana
Rouhani alisema siku ya Jumapili kwamba Wairani wana haki ya kuandamana na kutumia mamlaka yao lakini hatua zao hazipaswi kusababisha ghasia, fujo na kuharibu mali za watu. Muandamanaji mjini Tehran Mohammad Hossein Vakili amesema waandamanaji wako makundi mawili.
"Waandamanaji wamegawanyika katika makundi mawili. kundi moja linaandamana kwa kweli na lingine linafanya ghasia. kitu cha kwanza serikali inapaswa kuweka mipaka kati ya waandamanaji na wafanyaghasia. Ni jukumu zito na sijui, lakini viongozi wa juu wa serikali wanapaswa kutafuta suluhisho. Wasitoe adhabu kwa wahalifu na watu wasio na hatia bila kutenganisha. Kwanini wanikamate mtu kama mimi wakati naandamana kwa kupinga kupanda bei ya mayai?"
Erdogan amemwambia Rouhani , kwamba anayaona matamshi yake juu ya waandamanaji kutokiuka sheria wakati wakitekeleza haki yao ya kuandamana kwa amani kuwa ni sahihi," chanzo hicho kimesema.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Ulrike Demmer amesema serikali yake inaona kuwa ni haki wakati watu wakiandamana mitaani kupinga matatizo yao ya kiuchumi na kisiasa kama ilivyotokea nchini Iran kama ilivyo tokea na tunawaheshimu.
Wakati huo huo rais Donald Trump amesema kwamba ataonesha uungaji wake mkono kwa waandamanaji nchini Iran katika wakati muafaka, ikiwa ni matamshi yake ya hivi karibuni kabisa kupitia ukurasa wa Twitter.
Lakini kamanda wa jeshi la mapinduzi nchini Iran Mohammed Ali amesema maandamano ya wanaoipinga serikali nchini humo yamemalizika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman