Maandamano ya kupinga uwekezaji wa bandari Tanzania yazimwa
19 Juni 2023Maandamano hayo yaliyoratibiwa na Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, Deusdedith Soka, hayakuweza kufanyika kama ilivyopangwa baada ya Jeshi la Polisi, kuzuia na baadhi ya wanaharakati hao kukamatwa huku wengine wakishindwa kujitokeza katika maandamano hayo.
Juhudi za kumpata Soka hazikufua dafu kutwa nzima ya leo na badala yake, DW ilizungumza na mmoja wa waratibu wa maandamano hayo, Yoram Sethy, ambaye amesema, alishuhudia wenzake 11wakiwa chini ya ulinzi wa polisi eneo la Mnazi Mmoja.
Kwa mujibu wa Yoram, maandamano hayo yalipangwa kuanzia Mwembe Yanga, kisha Keko na baadaye Ikulu lakini baadaye walibadili utaratibu na kuamua kuanzia Mnazi Mmoja ambako wenzake walikamatwa.
Jana Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, liliyapiga marufuku maandamano hayo, na kuwataka wananchi kutoshiriki.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, naye amekazia marufuku hiyo leo akiwataka wananchi kutoshiriki maandamano hayo ambayo amesema hayana tija kwa taifa kwa sasa.
Chalamila amesema serikali ya Tanzania ina uungwana wa kufafanua jambo kwa undani endapo kuna mtu anahitaji ufafanuzi, na pia amesema kinachotafutwa si maandamano bali ni wenye nia mbaya wanaowatumia vijana kupeperusha ajenda zao.
Akizungumzia maandamano hayo, Mwanaharakati wa masuala ya siasa na aliyekuwa mjumbe wa Katiba Mpya, Deus Kibamba amesema maandamano ya sasa Tanzania yamepoteza maana.
Kumekuwa na maswali lukuki kuhusu mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji wa bandani kati ya kampuni ya DP World ya Dubai na Tanzania, na wanaharakati wa haki za binadamu, wakiwamo wanasiasa na viongozi wa dini, wameonyesha wasiwasi kuhusu mkataba huo.
Florence Majani. DW. Dar es Salaam.