1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya PEGIDA yapingwa

Mjahida6 Januari 2015

Maelfu ya Wajerumani jioni ya jana walishiriki kwenye maandamano katika miji mbalimbali kupinga maandamano ya kundi lijiitalo PEGIDA linalokosoa kusambaa kwa Uislamu nchini Ujerumani na kuongezeka kwa wageni.

https://p.dw.com/p/1EFUH
Maandamano ya kupinga vuguvugu la PEGIDA
Maandamano ya kupinga vuguvugu la PEGIDAPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Polisi inasema katika mji mkuu, Berlin, waandamanaji wapatao 5,000 waliwazuia waandamanaji 300 wa vuguvugu lijiitalo Wazalendo wa Ulaya Dhidi ya Usilimishwaji wa mataifa ya Magharibi kwenye lango maarufu la Brandenburg.

Waandamanaji wengine 22,000 waliripotiwa kushiriki kwenye maandamano ya kuwapinga PEGIDA katika miji ya Stuttgart, Münster na Hamburg.

Akizungumza kwenye mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Neustrelitz katika hafla ya chama cha CDU kuadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lorenz Caffier, hapo jana, Kansela Angela Merkel, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa PEGIDA, aliwashukuru wale waliomiminika mitaani dhidi ya PEGIDA:

"Hamutetereki linapokuja suala la kupigania uvumilivu na uhuru. Ninataka kusema tena kwamba kujitolea kwenu dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia hakuna shaka kabisa na ni jambo lenye thamani sana kwenye nchi hii.

Mataa ya kanisa kuu la mji wa Köln, yazimwa kupinga maandamano ya PEGIDA
Mataa ya kanisa kuu la mji wa Köln, yazimwa kupinga maandamano ya PEGIDAPicha: Reuters/Wolfgang Rattay

Kwa sababu tunapaswa kuinua bendera na kusema kwamba siasa kali za mrengo wa kulia, chuki dhidi ya wageni, chuki dhidi ya mayahudi hazina nafasi kwenye jamii," allisema Kansela Angela Merkel.

Vuguvugu la PEGIDA lasema ukosoaji wao ni wa halali.

Hata hivyo, waungaji mkono wa vuguvugu la PEGIDA walikaidi wito wa hapo kabla wa Kansela Merkel, Rais Joachim Gauck na hata makansela wa zamani kama vile Helmut Köhl na Gerard Schröder, na badala yake wakajitokea kwa wingi mjini Dresden kwenye ngome yao kuu, hapo jana. Polisi inakisia kiasi cha waandamanaji 18,000 walishiriki maandamano hayo ikiwa ni idadi ya juu kidogo kulinganisha na yale ya mwisho ya tarehe 22 Disemba.

Mjini Cologne, licha ya kuzimiwa mataa ya Kanisa Kuu la mji huo, mjumbe wa kamati ya uratibu ya PEGIDA, Kathrin Örtel, aliwaambia waandamanaji wake wasiofikia 300 kwamba wanasiasa wa Ujerumani wamelipotosha vuguvugu lao.

"Nadhani hivi sasa nchini Ujerumani tunashuhudia ukandamizaji wa kisiasa. Utafikiriaje vyengine ikiwa tunatukanwa au kuitwa wabaguzi au Wanazi na vyama vyote vikuu vya kisiasa na vyombo vya habari kwa sababu ya ukosoaji wetu halali dhidi ya sera ya kuomba hifadhi ya Ujerumani na kukosekana kwa sera ya uhamiaji," alisema Kathrin Örtel.

Waandamanaji mjini Köln
Waandamanaji mjini KölnPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Meya wa mji wa Cologne aliwaongoza maelfu kwa maelfu ya waandamanaji wanaowapinga PEGIDA kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la mji huo, maarufu kama Cologne Dom, ambalo mataa yake yalizimwa, kama ilivyokuwa kwenye majengo mengine kadhaa maarufu kote Ujerumani, kama ishara ya kupinga kile kinachotajwa kama upandikizaji wa siasa kali za kibaguzi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga