1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Zambia mjini Lusaka

Dennis Moyo17 Mei 2005

Wanafunzi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Zambia wamekamatwa jana baada ya kufanya maandamano yenye ghasia katika barabara kuu iendayo uwanja wa ndege. Barabara hiyo ilikuwa itumiwe na Rais Levy Mwanawasa wakati akitoka ziara ya nje.

https://p.dw.com/p/CHgr

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi hao, baada ya madai yao ya kutaka nyongeza ya asili mia kwa mia ya fedha za chakula na za kufanya utafiti kukataliwa na wizara ya elimu.

Kulingana na msemaji wa polisi mjini Lusaka, Bi Brenda Muntemba, wanafunzi hao walirushia mawe magari na wapita njia waliokuwa wakirudi majumbani baada ya saa za kazi. Hata hivyo hakutaja idadi ya wanafunzi waliokamatwa.

Katibu mkuu wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu, Chino Chileshe, amedai kuwa wanafunzi wamelazimika kufanya maandamano baada ya serikali kutosikiliza madai yao ya nyongeza ya fedha za chakula kutoka Kwacha 225,000 kwa mwezi ambazo ni sawa na dola za marekani 47 hadi Kwacha elfu mia nne ambazo ni sawa na dola za marekani 82.

Pia wanafunzi wa chuo kikuu cha Zambia wanadai wapewe Kwacha 800,000 ambazo ni sawa na dola za kimarekani 164 kwa ajili ya kufanyia utafiti. Kwa sasa wanapewa dola 80 tu ambazo mara ya mwisho ziliongezwa miaka kumi iliyopita.

Wanafunzi wanadai kuwa gharama ya maisha imepanda na serikali imekuwa ikiongeza mishahara katika idara nyingine wakiwasahau wanafunzi wa chuo kikuu.

Kwa sasa bei ya petroli mbayo ndiyo kigezo cha kupima kupanda kwa maisha, hivi majuzi imeongezeka mara dufu katika kipindi cha miezi sita iliyopita na kuwa lita moja inauzwa dola moja na senti 20 kwa lita.

Chuo kikuu cha Zambia ambacho kiko barabara kuu inayoelekea uwanja wa ndege wa kimataifa, iliwashawishi wanafunzi watake kuonana na msafara wa rais Levy Mwanawasa uliokuwa ukitokea uwanja wa ndege wa kimataifa kuelekea Ikulu baada ya ziara ya siku nne nchini Ghana na Libya. Hata hivyo msafara wa rais uliepusha njia na kutumia barabara nyingine hadi Ikulu kwa usalama.

Leo asubuhi, polisi wa kutuliza ghasia bado wamekuwa wakionekana maeneo ya chuo kikuu kujaribu kuzima maandamano mengine yoyote yale lakini hadi wakati ripoti hii inatumwa, hali ilikuwa shwari katika maeneo ya chuo kikuu.