1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yakithiri Marekani

Mjahida30 Aprili 2015

Maelfu ya watu wameandamana katika miji mikubwa nchini Marekani, wakitaka polisi kutoa huduma sawa kwa wote, hii ni baada ya kijana mmarekani mweusi kufariki kufuatia majeraha aliyoyapata akiwa mikononi mwa polisi.

https://p.dw.com/p/1FI5T
Watu waandamana kupinga kifo cha Freddie Gray
Watu waandamana kupinga kifo cha Freddie GrayPicha: Reuters/S. Stapleton

Maandamano makubwa yalionekana mjini Baltimore kwenyewe ambako ni kitovu cha ghasia za hivi maajuzi wakati vijana wengine wengi hasa wanafunzi walipofunga barabara na kuvuruga shughuli mjini humo.

Aidha maandamano mengine yamefanyika mjini New York, Washington, Boston, huku hasira zikiendelea kupanda miongoni mwa waandamanaji wanaopinga kile wanachokiita ukatili unaofanywa na maafisa wa polisi dhidi ya watu weusi pamoja na ubaguzi.

Waandamanaji hao waliojumuisha wamarekani weupe na weusi walibeba mabango huku wakisema kwa sauti, "Bila haki, hakuna amani! hakuna ubaguzi, hakuna amani!" "mikono juu usipige risasi " hii ikiwa inarejelea mauaji ya Michael Brown aliyeuwawa na polisi mwaka uliopita mjini Ferguson Missouri.

Waandamanaji mjini Baltimore
Waandamanaji mjini BaltimorePicha: Reuters/B. Snyder

"Tunaandamana kupinga dhuluma inayoendelea iliyoanzishwa na polisi dhidi ya watu weusi, tunahitaji kusitisha hilo," alisema Jonathan Brown, mwanafunzi aliye na miaka 19, anayesomea chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Kwa upande wake seneta wa jimbo la Maryland Catherine Pugh, amesema wataendelea kukemea visa vya ubaguzi hadi pale haki itakapo patikana.

"Hatutapumzika. Hatutapumzika hadi tupate haki ya Freddie Gray. Hatutapumzika hadi kuwe na uchunguzi wa wazi katika idara za polisi pamoja na polisi waliohusika katika mauaji ya Freddie Gray," alisema seneta Catherine Pugh.

Hata hivyo maandamano hayo yalikuwa ya amani na yaliyoendeshwa vizuri ingawa polisi mjini New York imesema imewakamata zaidi ya waandamanaji 60. Watu hao walikamatwa pale maandamano yalipoingia barabarani na kuanza kuvuruga usafiri wa magari.

Maafisa zaidi wa Usalama wapelekwa Baltimore kudhibiti hali

Kwa sasa maafisa wa polisi 2000 wametawanywa mjini Baltimore kuhakikisha amri ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja subuhi inaheshimiwa.

Jana Jumatano ilikuwa siku ya pili ya kutekelezwa kwa amri hiyo iliotolewa na meya wa mji huo Stephanie Rawlings-Blake. Amri hiyo iliwekwa baada ya vijana kumiminika barabarani baada ya mazishi ya Freddie Gray na kuanza kuzua vurugu huku wakichoma magari, kupora biashara za watu na kusababisha uharibifu mkubwa.

Polisi waliopelekewa mjini Baltimore kudhibiti hali
Polisi waliopelekewa mjini Baltimore kudhibiti haliPicha: picture alliance / ZUMA Press

Gray aliyekuiwa na miaka 25, alifariki baada ya kupata majeraha mabaya ya uti wa mgongo akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Hata hivyo utulivu umeripotiwa kurejea mjini humo. Wakati huo huo ingawa sababu iliopelekea kufariki kwa Freddie Gray haijajulikana maafisa sita wa polisi wamesimamishwa kazi kwa muda huku uchunguzi juu ya kifo hicho ukitarajiwa kuwasilisjwa kwa waendesha mashtaka wa mji huo siku ya Ijumaa.

Meya Stephanie Rawlings amesema majibu ya uchunguzi huo hayatatangazwa kwa umaah kwa hofu ya kutokea maandamano mengine.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Gakuba Daniel