Maandamano yaliyopangwa na wapinzani Tanzania yadhibitiwa
18 Aprili 2023Maandamano hayo yaliyoratibiwa na ngome ya vijana wa chama hicho yalikuwa na shabaha ya kuwasilisha kilio cha vijana kwa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuchelewa kuwajibishwa kwa vigogo wanaotajwa kuwa sehemu ya kuhujumu mali za umma kama ripoti ya CAG ilivyofichua katika ukaguzi wake hivi karibuni.
Vugugu la maandamano hayo ambayo ni ya kwanza kuratibiwa na kundi la vijana tangu kuondolewa marufuku ya shughuli za kisiasa, yalikuwa yamepanga kuanzia makao makuu ya chama hicho eneo la Magombeni na kisha kuzunguka katika mitaa kadhaa ikiwamo katikati ya jiji kabla ya kuhitimishwa ikulu ya Magogoni.
Soma pia: Tanzania: Majadala kuhusu ripoti ya CAG kufanyika bungeni Novemba
Lakini wakiwa wamejikunya katika ofisi za chama chao huku wakiwa wamenyanyua mabango yao, msafara wa maandamano hayo, ulidhibitiwa na askari polisi waliofika katika eneo hilo.
Mabishano yaliodumu kwa dakika kadhaa hayakuzaa matunda kwa vijana hao hali iliyowafanya baadhi yao kuruka rukua huku na kule huku wengine wakipiga miruzi na mayowe.
Soma pia: Tanzania: Ripoti ya CAG yazusha joto bungeni
Kiongozi wa ngome ya vijana wa chama hicho, Abdul Nondo ambaye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kuratibu maandamano hayo, aliamua kusoma risala iliyokuwa imekusudiwa kufikishwa kwa Rais Samia, ambako alibanisha namna wananchi wanavyovunjika moyo kutokana na ubadhilifu mkubwa unaotajwa kufanywa na watumishi wa umma.
Alisema huu siyo wakati tena wa kuendelea kuwafumbia macho wale wanaotajwa mara kwa mara kuhusika na vitendo vya namna hivyo na kusisitiza haja ya mkondo wa sheria kuwapitia watuhumiwa wa iana hiyo.
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe katika ujumbe wake wa twitter amepongeza hatua iliyoonyeshwa na vijana hao akisema wamedhubutu na kuonyesha ujasiri katika kulinda na kutetea rasilimali za taifa.,
Mjadala kuhusu ripoti ya CAG imekuwa mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari kila uchao ni hii huenda inachangizwa kutokana na madudu yanayotajwa kujirudia mara kwa mara huku wahusika wake wakiendelea kusalia kwenye nafasi zao.