Ubalozi wa Ujerumani nchini Libya wafungua tena milango
9 Septemba 2021Alipokuwa akiwa akizungumza baada ya kuwasili mjini Tripoli asubuhi ya Alhamisi, Waziri Maas amesema Ujerumani inataka kuwa na sauti nchini Libya, wakati nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikifanya juhudi kurejesha utangamano baada ya misukosuko ya kivita ya miaka ipatayo 20.
Ubalozi wa Ujerumani katika mji mkuu wa Libya, Tripoli ulifungwa mwaka 2014 wakati ghasia zilipokuwa zimepamba moto, na wanadiplomasia wake walihamishwa na kufanyia katika katika nchi jirani ya Tunisia.
Soma zaidi: Mwanawe Gaddafi aachiliwa huru Libya
Kulingana na tangazo la wizara ya mambo ya nje mjini Berlin, Waziri Heiko Maas amesifu hatua zilizopigwa nchini Libya kuelekea amani, zikiwemo kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta, na kwa kiasi kikubwa, kunyamazishwa kwa milio ya silaha.
Ujerumani kama mpatanishi katika mzozo wa Libya
Maasi ameongeza kuwa Libya inahitaji ushirikiano wa kudumu na jumuiya ya kimataifa, ili kufikia malengo ya maendeleo kwa Walibya wote.
Kwa muda mrefu Ujerumani imekuwa ikibeba jukumu la upatanishi katika mzozo wa Libya. Mwezi Juni mwaka huu, kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa, Ujerumani iliandaa mkutano mjini Berlin uliojadili mustakabali wa taifa hilo lililosambaratishwa na vita.
Soma zaidi:Mjumbe wa UN Libya : Waharibifu wanajaribu kuzuia uchaguzi nchini Libya
Katika mkutano huo, Ujerumani iliahidi kuendeleza shinikizo hadi pale wapiganaji wote wa kigeni watakapokuwa wameondoka kwenye ardhi ya Libya.
Umoja wa Ulaya kusaidia mchakato wa uchaguzi wa Libya
Huku hayo yakiarifiwa, mkuu wa diplomasia katika Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema umoja huo uko tayari kusaidia zaidi katika mchakato wa kuandaa uchaguzi mkuu wa Libya unaotazamiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.
''Umoja wa Ulaya ungependa kuisaidia Libya kwa uzoefu mkubwa ulioupata katika kuwasaidia washirika wengi katika kujenga miundo ya kitaifa wakati wa kipindi cha mpito,'' amesema Borrell na kuongeza kuwa ''tuko tayari kuipiga jeki Libya katika mipango ya kuzijengea uwezo taasisi zake za kitaifa na za ngazi ya chini.''
Borrell aliitoa ahadi hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Libya Najla al-Mangoush mjini Tripoli. Mwanadipolomasia mkuu huyo wa Ulaya alisema Libya haina muda wa kupoteza katika mchakato wa kuidhinisha sheria muhimu za uchaguzi wa bunge wa Desemba 24.
Uwezekano wa kucheleweshwa kwa uchaguzi
Mwezi Uliopita, waziri Mangoush alizungumzia uwezekano wa kuuchelewesha uchaguzi huo, ikiwa bunge litaendelea kujikokota katika kupitisha sheria hiyo muhimu ya uchaguzi.
Katika mazungumzo yao, waziri wa mambo ya nje wa Libya aliuomba Umoja wa Ulaya kuisaidia nchi yake katika maandalizi ya uchaguzi, na kuimarisha udhibiti wa mpaka wake wa kusini.
ape, afpe