1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maasi ya Darfur: Ushahidi waanza kutolewa ICC

24 Mei 2021

Ushahidi dhidi ya kiongozi wa kundi la janjaweed  Ali Mohammed Ali Abdul Rahman lilinalolaumiwa kwa kutekeleza maasi Darfur, nchini Sudan waanza kutolewa katika Mahakama ya ICC siku ya Jumatatu .

https://p.dw.com/p/3tssd
Niederlande Den Haag |  Fatou Bensouda Chefanklägerin Internationaler Strafgerichtshof (ICC)
Picha: picture-alliance/AA/A. Asiran

Kiongozi wa kundi hilo ambaye pia anajulikana kwa jina la Ali Kushayb, anakabiliwa na mashtaka 31 ya uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na uhalifu wa kivita unaojumuisha  mauaji, ubakaji na mateso.

Bado hajajibu kuhusu mashtaka hayo lakini wakati wa kikao cha mwaka jana,aliwaambia majaji  wa mahakama hiyo ya ICC kwamba madai hayo sio ya kweli. Wakili wake Cyril Laucci, anapinga mamlaka ya mahakama hiyo katika  kesi hiyo.

Flüchtlinge in Darfur
Wakimbizi katika kambi ya Abu Shouk waliotoroka ghasia za kundi la JanjaweedPicha: AP

Wakati wa kutolewa kwa ushahidi wa kwanza katika kikao cha leo katika mahakama hiyo ya kimataifa ya ICC, kiongozi mkuu wa mashtaka hiyo Fatou Bensouda, aliwaambia majaji wa mahakama hiyo kwamba Abdul Rahman alifanya maovu hayo kwa kufahamu na kujitolea na kwamba alitekeleza jukumu muhimu la kuongoza katika mashambulizi na kuagiza mauaji mengine.

Ushahidi zaidi wa Bensouda

Bensouda amesema kuwa vikosi vya wanamgambo wa Janjaweed hutumia ubakaji kama silaha ya kuwahangaisha na kuwadhalilisha wanawake na kuelezea kisa cha mwanamke mmoja aliyekamatwa na mpiganaji wa kundi hilo na kubakwa huku akiwa ameshikiwa kisu. Bensouda aliwaambia majaji hao kwamba mwathiriwa huyo ambaye pia ni shahidi katika kesi hiyo alisema kuwa alipiga kelele na mpiganaji mwengine akaja na upanga aliomuwekea mdomoni na kumwambia atamkata iwapo ataendelea kupiga kelele.

Umuhimu wa kikao cha leo

Kikao cha leo sio cha kusikiliza kesi. Badala yake, kinanuiwa kubainisha iwapo ushahidi ulioko dhidi ya Abdul Rahman unatosha kumfungulia kesi katika mahakama hiyo ya kimataifa. Uamuzi kuhusu ushahidi huo unatarajiwa baadaye mwaka huu.