1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maaskofu wataka uchaguzi wa huru na haki Tanzania

10 Septemba 2020

Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania wameonya kuhusu wimbi la matukio ya rushwa na vitendo kama baadhi ya wagombea kunyimwa fursa kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu nchini humo

https://p.dw.com/p/3iHq5
Tansania Wahlen
Picha: Reuters/S. Said

Wakati viongozi hao wakitahadharisha hayo, wagombea mbalimbali wa urais na ubunge wameendelea kuchuana kwenye majukwaa ya kampeni kila mmoja akijaribu kuvutia upande wake. Ikiwa sasa wanakaribia kumaliza wiki ya pili tangu wagombea hao wajitupe kwenye majukwaa ya kampeni, viongozi wa dini hawajajiweka kando katika uchaguzi huu wakitoa rai kuhusu yale wanayosema kuwa yanapaswa kukemewa kabla ya uchaguzi wenyewe haufajanyika. Saoma zaidi: Tanzania yaihakikishia Marekani uchaguzi utakuwa huru

Miongoni mwa mambo ambayo wamekuwa wakiyataja kwenda kombo ni yale yanayowahusu baadhi ya wagombea na wapiga kura kuwekeana makubaliona yenye sura ya rushwa.

Tansania Palamagamba Kabudi, Außenminister & Donald Wright, US-Botschafter
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania na MarekaniPicha: Courtesy of Ministry of Foreign Affairs

Akilizungumzia jambo hilo, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Arusha, Askofu Isaac Amani Massawe amesema uchaguzi ni tukio muhimu linalofanyika mara moja baada ya kipindi fulani, hivyo mwananchi anayo haki kumchagua kiongozi anayemkubali katika hali ya uhuru, uwazi na ukweli bila kurubuniwa kwa jambo lolote.

Suala la baadhi ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kuenguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho limewashtua pia viongozi hao wa dini ambao wanasema safari hii limevuka mipaka. Idadi kubwa ya wanasiasa hao walioenguliwa wamekata rufaa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imeanza kusikiliza rufaa hizo. Soma zaidi: Vyama vya siasa Tanzania vyaanza kunadi sera zao

Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Askofu Severine Niwemugizi anasema mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu unapaswa kufanywa kwa kuzingatia haki bila kuweka nukta yoyote ya upendeleo ili maoni ya wananchi yasikike kupitia sanduku la kura.

Tansania CHADEMA in Dar es Salaam
Msafara wa wafuasi wa CHADEMA Dar es SalaamPicha: DW/S. Khamis

Wakati huu ambako Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiendelea kutoa orodha ya rufaa ilizozitolea maamuzi, wagombea wa urais pamoja na wale wa ubunge wameendelea kuchuana katika majukwaa ya kisiasa kwa kunadi sera zao.

Chama tawala CCM, kimewatawanya makada wake katika maeneo mbalimbali huku mgombea wake wa urais akiendelea na kampeni katika eneo la Kanda ya Ziwa, wakati mgombea wake mwenza yuko mkoa wa Lindi. Soma zaidi: HRW: Uhuru mashakani kuelekea uchaguzi Tanzania

Naye mgombea wa chama kikuu cha upinzani Chadema, ambaye leo alipanga kuanza awamu ya pili ya kampeni zake akianzia huko Pwani ameshindwa kufanya hivyo. Taarifa ya chama hicho imesema kampeni ya Tundu Lissu imevurugika baada ya helikopta aliyokuwa atumie kufika katika maeneo ya kampeni kuzuiliwa kwa kunyimwa kibali na mamlaka zinazohusika.

George Njogopa, DW Dar es Salaam