Mabao 37 yatinga wavuni wiki ya kwanza Bundesliga
12 Agosti 2013Mchezo wa kwanza wa msimu wa 51 katika Bundesliga , mashabiki wameshuhudia mabao 37 yakitinga wavuni. Schalke 04 na Hamburg SV zilitoshana sare ya mabo 3-3 jana Jumapili(11.08.2013).
Mainz 05 ilipata ushindi katika mchezo mwingine jana dhidi ya VFB Stuttgart wa mabao 3-2.
Mabingwa wapeta
Mabingwa watetezi Bayern Munich walipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Borussia Moenchengladbach ambapo mabingwa hao walipata penalti mbili katika kipindi cha dakika 1.30. Mlinda mlango wa mabingwa hao watetezi manuel Neuer amesema wameridhika na mchezo wao.
"Tumeridhika. tumepata mabao mawili yakuongoza na mapema. Na kisha tukajifunga bao wenyewe kupitia Dante. tumepoteza hata hivyo nafasi nyingi za kufunga mabao. Lakini kwa jumla tuliweza kuthibiti kila kitu na yalikuwa matokeo mazuri".
Nao makamu bingwa Borussia Dortmund ilizoa point tatu zote kwa ushindi wa kishindo wa mabao 4-0 dhidi ya FC Augsburg , na mshambuliaji Aubameyang akianza Bundesliga kwa kishindo kwa kupachika mabao 3.Mlinzi wa Dortmund Neven Subotic alimwagia sifa mshambuliaji wa timu hiyo Aubameyang.
"Ni kitu cha kipekee kwa Aubameyang , ulikuwa mchezo wa aina yake. Matokeo ya mchezo huo pamoja na mabao aliyofunga , amefanya kazi nzuri sana na tulimsaidia vizuri kutimiza hilo. Tulicheza vizuri na kupambana kwa kiwango cha juu na tulistahili kushinda".
Kipigo cha mbwa mwizi
Katika mchezo huo wa wiki ya kwanza ya Bundesliga , timu iliyorejea katika daraja la kwanza msimu huu Hertha BSC Berlin inashikilia usukani kwa kutumbukiza wavuni mabao mengi, ambapo iliisambaratisha Eintracht Frankfurt kwa mabao 6-1 na kumshangaza hata kocha wao Jos Luhukay. Kama anavyosema mchezaji wa kiungo wa Hertha john Brooks.
"Tumeuchukulia ushindi huu kwa unyenyekevu. Kwasababu umetufanya tujisikia furaha, si jambo la kawaida. Si kila wiki timu inaweza kushinda mabao 6-1. Kwetu sisi ni mafanikio makubwa kwa kuanza msimu. Kwa mashabiki wetu wakituunga mkono ilikuwa furaha kubwa. Wanaposema wiki ijayo tuendelee kufanya hivyo , naungana nao moja kwa moja".
Michezo ya kirafiki
Wakati huo huo Bundesliga inapumzika kwa wiki moja kupisha michezo ya kirafiki ya kimataifa ya timu ya taifa. Ujerumani inapambana na Paraguay.
Michezo hiyo ya kirafiki ya kimataifa katika bara la Ulaya na kwingineko inaashiria mwanzo wa msimu ambao fainali za kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil zinakaribia.
Baadhi ya vigogo vya soka barani Ulaya vinapambana wenyewe kwa wenyewe wakati kuna mapambano kadha kati ya timu za bara la Ulaya dhidi ya timu kutoka bara la America ya kusini.
Mabingwa wa dunia Uhispania wanasafiri kwenda Ecuador, wakati Italia inatiana kifuani na Argentina na Ujerumani ina miadi na Paraguay.
Timu za mataifa kadha ya America ya kusini zimeamua kupambana na ama mataifa ya Ulaya ama ya Asia , ikiwa ni pamoja na wenyeji wa fainali za kombe la dunia Brazil ambayo inakibarua dhidi ya Uswisi mjini Basel.
Kwingineko Colombia inakutana na Serbia mjini Barcelona , Uruguay inapimana nguvu na Japan, Peru ikipima uwezo wake dhidi ya Korea ya kusini na Chile inakutana na Iraq nchini Denmark.
kuna mapambano yanayovuta hisia , wakati Uingereza ikipima kiwango cha uhasama kilichopo kati yake na Scotland, Ureno ikiikaribisha Uholanzi, na Ubelgiji dhidi ya Ufaransa na Sweden inapimana nguvu na ndugu zao wa Denmark.
Wakati huo huo mchezaji nyota chipukizi Julian Draxler hataweza kujiunga na wenzake katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani ambacho kitakuwa uwanjani siku ya Jumatano kupambana na Paraguay baada ya kuumia mguu katika mchezo wa ufunguzi wa Bundesliga, limesema shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB leo.
Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 mchezaji wa kati wa Schalke 04 amepata maumivu hayo katika mchezo kati ya timu yake na Hamburg SV jana Jumapili.
Ujerumani inashikilia nafasi ya kwanza katika kundi lake la kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia ikiwa na points 16 , point sita mbele ya Austria, ambayo inapambana nayo hapo Septemba 6 kabla ya kwenda katika visiwa vya Faroe siku nne baadaye. Sweden na Ireland katika kundi hilo zina points 11 kila moja.
Gabon kwenda Afrika kusini
Katika bara la Afrika Gabon imefanikiwa kufuzu kucheza fainali za kombe la Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani , baada ya kuipa kipigo Cameroon cha bao 1-0. Katika mchezo wa kwanza Cameroon ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gabon. Gabon ilishinda kwa mikwaju ya penalti 6-5 na kufuzu kuingia katika fainali hizo baada ya kutoka sare katika matokeo jumla kwa bao 1-1.
Gabon imefuzu kucheza katika fainali hizo zitakazofanyika Januari 11 nchini Afrika kusini na Cameroon sasa itapambana na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo wakiwania nafasi nyingine katika fainali hizo. Mchezo kati ya Zimbabwe na Zambia umeahirishwa hadi Agosti 18 na pia mchezo kati ya Msumbiji na Angola umeahirishwa hadi Agosti 25.
Usain Bolt
Mashindano ya ubingwa wa dunia wa Riadha yanaendelea mjini Moscow , ambapo jana(11.08.2013) mkimbiaji mbio fupi Usain Bolt aliwahakikishia mashabiki wake kuwa bado ni moto wa kuotea kwa mbali pale aliposhinda mbio za mita 100 kwa kutumia sekunde 9.77.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / ZR
Mhariri: Yusuf Saumu