1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabasi yaanza kuwaondoa raia kutoka vijiji tiifu kwa Syria

Sylvia Mwehozi
19 Julai 2018

Zoezi la kuwahamisha maelfu ya watu kutoka vijiji viwili ambavyo ni tiifu kwa utawala wa Syria na ambavyo vilikuwa chini ya mzingiro wa waasi kaskazini magharibi mwa nchi hiyo sasa limekamilika

https://p.dw.com/p/31jFV
Syrien Busse zum Transport von Flüchtlingen
Picha: Getty Images/AFP/O. H. Kadour

Televisheni ya taifa ya Al-Ikhbariya imeripoti kwamba mabasi yote yameondoka katika vijiji vya Fuaa na Kefraya asubuhi ya Alhamis, yakifanya vijiji hivyo viwili vya Washia kutokuwa na raia kabisa. Mabasi hayo yanasafiri kupitia eneo linaloshikiliwa na waasi na bado hayajawasili kizuizi cha serikali kilomet 30 kutoka vijiji hivyo.

Zaidi ya mabasi 100 yaliwasili jana jioni kwa ajili ya kuwasafirisha raia na wapiganaji usiku wa kumkia leo kutoka vijiji hivyo ambavyo viko karibu na eneo linaloshikiliwa na serikali kwenye jimbo la Aleppo. Zoezi la kuwahamisha lilianza kwa magari ya kubeba wagonjwa kuwakimbizi wagonjwa hadi kwenye kizuizi cha serikali kabla ya mabasi karibu 121 kuondoka vijijini hapo.

Syrien Busse zum Transport von Flüchtlingen
Moja ya mabasi yaliyowabeba raia na wapiganaji kutoka Fuaa na KafrayaPicha: Getty Images/AFP/O. H. Kadour

Televisheni ya Al-Ikhbariya imesema takribani magari 10 ya kubeba wagonjwa yaliondoka na wagonjwa walio katika hali mbaya. Vijiji hivyo vimekuwa chini ya mzingiro kwa miaka kadhaa na waasi wa Kiislamu wa Kisunni katika jimbo la Idlib, ambalo ni eneo kubwa lililosalia mikononi mwa waasi nchini Syria.

Rais Bashar al-Assad ambaye anazidi kusonga mbele dhidi ya waasi kaskazini magharibi, ameapa kuitwaa tena nchi nzima. Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia haki za binadamu la Syria, vijiji vya Fuaa na Kafraya vilikuwa vitupu bila ya raia karibu 7000 baada ya raia na wapiganaji kuondoka chini ya mapatano ya kuwahamisha.

Mapatano hayo yalifikiwa chini ya utawala wa Syria ukiungwa mkono na Urusi na waasi ambao ni washirika wa Uturuki. Chini ya makubaliano hayo, raia wote watapelekwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali kwa kubadilishana na wafungwa watakaoachiliwa na serikali.

Vijiji hivyo ambavyo vilikuwa vikikaliwa na idadi kubwa ya Washia, vilizingirwa na waasi na kundi la kijihadi la Hayat tahrir al-Sharn likiongozwa na mshirika wa zamani wa Al-Qaeda.

Syrien Zivilisten versuchen sich in Sicherheit zu bringen | Rashidin
Watoto wakiwa tayari kwenye mabasi kutoka vijiji vya Fuaa na KafrayaPicha: Getty Images/AFP/O. Haj Kadour

Fuaa na Kafraya yalikuwa ni maeneo yaliyokuwa yamesalia chini ya mzingiro Syria ambako vikosi vya serikali mara kadhaa vimetumia vizuizi vya barabarani katika vita iliyodumu miaka saba. Kuanzia siku ya Jumatano asubuhi vizuizi hivyo viliondolewa katika barabara ya kuelekea katika vijiji ili kuyaruhsu mabasi kupita.

Vikiwa vimezungukwa na kushambuliwa na vikundi vya wanamgambo vilivyogawika, vijiji hivyo vimekuwa ni mwito wa mshikamano kutoka kwa serikali na pia wakati huo huo ikiwa ni karata ya mchezo mikononi mwa waasi. Vilizingirwa tangu mwaka 2015 wakati waasi na wanajihadi waliovamia na kushikilia jimbo karibu la Idlib na kukata upatikanaji wa vyakula na madawa.

Majeshi hayo yaliwaruhusu Umoja wa Mataifa na shirika la kiarabu la Hilal nyekundi la Syria kusambaza misaada katika miji hiyo kwa kubadilishana na operesheni na miji miwili iliyozingirwa na serikali karibu na Damascus. Mnamo mwezi Aprili 2017, maelefu waliondolewa kwa mabasi kutoka Fuaa na Kafraya ili kubadilishana na zoezi kama hilo kutoka miji ya Zabadani na Madawa. Lakini bomu lililoulenga msafara kutoka Fuaa na Kafraya uliwaua watu takribani 150 wengi wao wakiwa raia  wakiwemo watoto 72.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Zainab Aziz