1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Machafuko mjini Jerusalem yazusha wasiwasi

5 Aprili 2023

Polisi ya Israel iliuvamia msikiti wa Al-Aqsa katika Mji wa Kale wa Jerusalem mapema leo, na kupambana na Wapalestina waliokuwa wakiwarushia mawe na fataki katika vurugu zilizozuka wakati wa msimu nyeti wa sikukuu.

https://p.dw.com/p/4PjwF
Kamatakamata ya polisi kwenye viunga vya msikiti wa Al-Aqsa
Makabiliano mapya kati ya jeshi la Israel na Wapalestina huko Jerusalem yamezusha wasiwasi wa kimataifa Picha: Mahmoud Illean/AP/picture alliance

Wanamgambo wa Kipalestina walijibu kwa kufyatua makombora kusini mwa Israel kutokea Ukanda wa Gaza, na kusababisha mashambulizi ya mfululizo ya kutokea angani ya Israel.

Kundi la Hamas linaloudhibiti Ukanda wa Gaza limetishia kuzuka kwa makabiliano mapya lakini afisa mmoja amesema Mamlaka ya Wapalestina inawasiliana na Misri, Jordan, Marekani na Umoja wa Mataifa ili kuutuliza mvutano.

Mapigano hayo yanayojiri wakati Waislamu wakiadhimisha mwezi wa mfungo wa Ramadhan na Wayahudi wakijiandaa kwa Siku kuu ya Pasaka, yamezusha hofu ya kutokea mvutano mpana.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake inafanya juhudi za kutuliza mivutano katika eneo hilo takatifu.