Hali ya wasiwasi imetanda katika Ukingo wa Magharibi
16 Oktoba 2015Katika eneo la ukingo wa Magharibi linalokaliwa kimabavu na Israel Wapalestina wenye hasira walichoma moto madhabahu ya Kiyahudi karibu na mji wa Nablus, na kumchoma kisu mwanajeshi wa Israel karibu na Hebron, wakati wasiwasi ukizidi kutanda kufuatia machafuko yaliyodumu kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Jeshi la Israel limesema karibu watu 100 walikusanyika kwenye kaburi la mtakatifu Joseph au Nabii Yusuf kama anavyojulikana kwa Waislamu, katika eneo la kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi na kuliwasha moto kabla ya kuwasili vikosi vya usalama vya Palestina na kuwarudisha nyuma.
Rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amelaani kitendo cha waandamanaji hao kuchoma madhahabu hayo, na kutaka yakarabatiwe haraka. Naye Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amelaani shambulizi dhidi ya madhabu hayo na kutaka waliohusika watafutwe na kushukuliwa hatua za kisheria.
Saa chache baadae, Mpalestina alievalia kama mwandishi habari alimjeruhi kwa kisu mwanajeshi wa Israel, kabla ya kupigwa risasi na kuuawa, limeongeza jeshi la Israel. Shambulizi hilo lilitokea karibu na Hebron, katika eneo la kusini la maeneo yanayokaliwa kimabavu.
Katika Ukanda wa Gaza, wizara ya afya ya ukanda huo ilisema watu wawili walifariki baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel. Msemaji wa wizara hiyo Ashraf al-Qudra alisema Abdul Qadir Farhat, mwenye umri wamiaka 19, alifariki baada ya kupigwa risasi kichwani katika makabiliano karibu na kivuko cha Beit Hanoun, kaskazini mwa Gaza.
Mahmud Homaida, 22, alithibitishwa kufariki baadae katika makabiliano mpakani mwa Gaza na Israel. Wizara ya afya imesema watu wengine 98 walijeruhiwa, wakiwemo waliopigwa risasi au kushambuliwa kwa mabomu ya machozi.
Siku ya Ghadhabu
Vuguvugu la Hamas, linalotawala katika ukanda wa Gaza, liliitisha maandamano ya siku ya Ghadhabu siku ya Ijumaa, ambapo naibu kiongozi wa vuguvugu hilo Ismail Haniya alisema uasi mpya wa Wapalestina dhidi ya Israel ndiyo umeanza na utaendelea.
Matamshi yake yalitangazwa kupitia televisheni ya Hamas ya Al-Aqswa iliyoko mjini Gaza, ambapo alisema Intifadha hiyo inapaswa kuwa ya vurugu zaidi ili kulinda Jerusalem na msikiti wa Al-Aqswa, ambao ndiyo eneo la tatu kwa utakatifu katika dini ya Kiislamu.
Jumla ya Wapalestina 36 wameuawa mpaka sasa tangu kuanza kwa machafuko hayo mwezi uliyopita, wakiwemo wanaodaiwa kuwa washambuliaji. Mamia wengine wamejeruhiwa na kwa upande mwingine Waisrael saba wameuwa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi ya visu, silaha na magari.
Mamia ya Wapalestina wamekabiliana na vikosi vya Israel katika maeneo tofauti ya mpaka wa nchi hiyo na Gaza, baada ya Hamas kuitisha maandamano hayo ya ghadhabu.
Baraza la usalama lakutana
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekutana mjini katika kikao maalumu kujadili hali katika eneo hilo. Naibu balozi wa Israel aliwashtumu Wapalestina kwa kuuwa raia wasio na hatia, huku akisema nchi yake haiko tayari kukubali waangalizi wa kimataifa kwenye eneo la Temple Mount.
"Naomba niwe muwazi kabisaa --- Israel haitakubaliana kwa namna yoyte ile, juu ya kupelekwa waangalizi wa kimataifa kwenye Mlima Temple. Uwepo kama huo utakuwa mabadiliko katika hali ya sasa," alisema naibu balozi huyo David Roet.
Machafuko yamechochewa kwa sehemu na hasira za Wapalestina juu y akile wanachokiona kama hatua ya Mayahudi kuzidi kuusogelea msikiti mtakatiku wa al-Aqswa, ambao pia unatukuzwa na Wayahudi kama eneo la hekalu mbili za Wayahudi zilizoharibiwa, zinazotajwa kwenye Biblia.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, amesema anapanga kuizuru mashariki ya Kati kujaribu kutuliza ghasia. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Nyetanyahu amesema yuko tayari kukutana na rais Mahmoud Abbas kusaidia kurejesha utulivu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.