1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar: Salva Kiir kikwazo cha kupatikana amani Sudan Kusini

Jane Nyingi
18 Oktoba 2016

Makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini, Riek Machar, amemshtumu Rais Salva Kiir kwa kuendelea kuhujumu juhudi za kupatikana amani Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/2RLMs
Südsudan Riek Machar Rebellenführer
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Ayene

Katika mahojiano ya moja kwa moja na DW, Machar ambae sasa hivi yuko nchini Afrika kusini kwa matibabu ameitaka jamii ya kimataifa kuingia kati ili kuzuia mauji zaidi.

Tukio la hivi punde ni la mauaji ya zaidi  ya watu 50 kufuatia mapigano nje ya mji wa Malakal kati ya majeshi ya serikali na  yale yanayounga mkono Riek Machar. Msemaji wa jeshi la serikali Lui Ruag Konag amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka na kufikia watu 80. Akizungumzia mashambulizi hayo akiwa nchini Afrika kusini, Machar amesema hali inayoshuhudiwa sasa Sudan Kusini imechangiwa pakubwa na Rais Kiir, kwani tangu mwanzo alionyesha kutokuwa makini kufanikisha utekelezaji makubaliano ya kurejesha amani nchini humo. Hali hiyo anasema ndio hata iliyochangia mapigano ya tarehe 8 mwezi Julai mwaka huu yaliyomlazimu kutoroka mjini Juba na kuingia nchini Kongo kupitia eneo la mpakani. “Ni hali ya kusikitisha, ni ya kusikitisha kwa sababu watu zaidi wanaendelea kujeruhiwa na wengine kuyatoroka makaazi yao. Hivi sasa zaidi ya raia million moja wa Sudan Kusini wametafuta hifadhi mataifa jirani  na idadi hii huenda ikaongezeka, hivi ni vita vilivyolazimishwa kwetu, sisi tunajikinga.”

UNHCR Südsudan Flüchtlinge
Raia wa Sudan Kusini waliotorokea UgandaPicha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Machar amekanusha madai ya serikali kuwa aliingia katika mkutano uliokuwa umetishwa na Rais Kiir akiwa na bastola wakati wa kutokea machafuko hayo ya tarehe 8  mwezi julai na kusema hizo zilikuwa njama za kumchafulia jina.“Kwanza huu ni uwongo mtupu mimi nialicha kubeba bunduki mwaka 1991 nilipoacha kuwa kamanda. Nilishangazwa na madai  hayo kuwa rais alisema nilienda mkutano huo nikiwa nimejihami kwa bastola, yeye ndiye aliyeitisha mkutano kwa nini nije  na bastola, ni yeye aliyekuwa na nia mbaya dhidi yangu. Mimi nataka kusisitiza si kweli”

Südsudan Schüsse während PK im Präsidentenpalast
Ikulu ya rais,baada ya kusikika milio ya risasiPicha: picture alliance/dpa

Hata hivyo ameitaka jamii ya kimataifa kuingia kati ili hali kurejea kawaida Sudan Kusini. Kwa upande wake ujumbe wake ni huu:“Tunataka kumaliza vita hivi haraka iwezekanavyo,lakini tatizo hatujapata nafasi ya kushiriki mazungumzo,tumebaki bila namna ila kukabiliana na utawala wa kidiktator ili kujilinda na pia wakulinda raia wa Sudan kusini”

Machar ameshikia ataendelea kushiriki  siasa licha ya serikali  ya Juba kutangaza  imempiga marufuku.

 

Mwandishi: Jane Nyingi/AfricaLink
 

Mhariri: Mohammed Khelef