Macron amsifu Abiy kwa mageuzi ya kihistoria Ethiopia
30 Oktoba 2018Rais Emmanuel Macron ameyataja mageuzi ya waziri mkuu huyo kijana mwenye umri wa miaka 42 kuwa yasiyotarajiwa. Abiy yuko katika ziara yake ya kwanza barani ulaya tangu aliposhika wadhifa huo mwezi Aprili baada ya kujiuzulu ghafla mtangulizi wake Hailemariam Desalegn mwezi Februari..
Amepongezwa takriban na wengi ulimwenguni kwa jitihada zake za kuleta amani na taifa jirani la Eritrea, kutangaza mageuzi ya kuchumi na kuwanyooshea mkono wa maridhiano wapinzani ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru maelfu ya wafungwa wakiwemo wa kisiasa, kuviruhusu tena vyama vya kisiasa vilivyopigwa marufuku na kuahidi uchaguzi huru na wa haki 2020, ingawa bado anakabiliana na mizozo ya kikabila iliosababisha watu milioni 1.4 kuyahama makazi yao.
Akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Paris akiwa pamoja na kiongozi huyo wa Ethiopia, Rais Macron alisema Ufaransa inaziunga mkono juhudi zake za kuleta mabadiliko nchini Ethiopia na akamwambia Dr Abby, "hapa una nchi inayoipenda nchi yako na kuvutiwa pia na mageuzi unayoyatekeleza."
Macron akaongeza kusema kwamba anafahamu changamoto kubwa aliyokabiliana nayo Waziri mkuu Abiy katika kuleta mabadiliko hayo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, akisema ni jambo lisilo tarajiwa.
Ufumbuzi kupitia amani na maridhiano
Kwa upande wake kiongozi huyo wa Ethiopia aliahidi kutatua migogoro na mapigano ya kikabila , akisema ufumbuzi utapatikana kwa maridhiano na kupigania amani na anaamini mabadiliko yataleta suluhisho."
Akamtaka Macron kutoa mchango mkubwa katika juhudi za kuimarisha amani kati ya Eritrea na Djibouti, ambazo zilikubaliana mwezi uliopita kurejesha uhusiano wao katika hali ya kawaida baada ya muongo mmoja wa mzozo wa mpaka uliosababisha mapigano ya muda mfupi kati yao.
Ufaransa na Ethiopia zimesaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika nyanja mbali mbali kuanzia usafiri hadi nishati na utamaduni.
Waziri mkuu Abiy Ahmed, amegeuza nchi yake Ethiopia kuwa ya kwanza barani Afrika, kuleta mageuzi ya uongozi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika baraza la mawaziri , idadi sawa kati ya wanaume na wanawake. Mnamo wiki iliopita wabunge mjini Addis Ababa walimuidhinisha rais wa kwanza mwanamke nchini humo, na ambaye kwa wakati huu ndiye mkuu pekee wa taifa aliye mwanamke barani Afrika .
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ap,afp
Mhariri: Yusuf, Saumu