1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron asema Uturuki ni mshirika muhimu

Sekione Kitojo
7 Septemba 2017

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema Uturuki inabaki kuwa mshirika muhimu wa Umoja wa Ulaya na mahusiano yanapaswa kuendelezwa hata kama nchi hiyo imetoka kutoka katika njia ya Umoja huo.

https://p.dw.com/p/2jX53
Frankreich Türkei Präsidenten Emmanuel Macron und Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/AP Images/E. Feferberg /Pool

Uturuki  na  Ujerumani ambao  ni  washirika  katika  Jumuiya  ya NATO wameshambuliana  kwa  maneno makali, katika  muda  wa miaka  miwili . Lakini Umoja  wa  ulaya  kwa  jumla umeshitushwa  na hatua za  ukandamizaji  za  rais Tayyip Erdogan dhidi  ya  wapinzani kufuatia  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi  nchini  Uturuki  Julai mwaka  jana.

Kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel aliimarisha  msimamo  mkali kuhusiana  na  juhudi  za  Uturuki  zilizokwama  kwa  muda  mrefu katika  mdahalo  wa  televisheni  Jumapili  iliyopita pamoja  na mgombea  mwenzake  katika  uchaguzi  wa  taifa  unaotarajiwa kufanyika  Septemba  24.

Frankreich Migrationsgipfel in Paris
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron(kushoto)Picha: Reuters/C. Platiau

Afisa  mwandamizi wa  Uturuki  amesema  mataifa  ya  Umoja  wa Ulaya  yanapaswa  kuamua  iwapo wanaitaka  Uturuki  kuwa mwanachama  ama  la, lakini  kuna  hisia "kwamba  hawataki  tena ndoa , bali  wanataka  kuishi  pamoja  tu.

Matamshi  ya  rais  wa  Ufaransa  Macron  yanafuatia  matamshi  ya kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel  kwamba  Umoja  wa  Ulaya unapaswa  kusitisha  kabisa  mazungumzo  na  Ankara.

"Ni  kweli  kwamba  Uturuki imetoka  nje ya  njia  ya   Umoja  wa Ulaya   katika  miezi  ya  hivi  karibuni  na  kinachotia  wasi  wasi zaidi  ni  ukiukaji kwa  njia  ambayo  haiwezi kupuuzwa," Macron ameliambia  gazeti  la  Ugiriki  la  Kathimerini.

"Lakini nataka  kuepuka  kuvunjika, kwasababu  ni  ni  mshirika muhimu  katika  mizozo  mingi  ambayo  tunakabiliana  nayo, hususan changamoto  za  uhamiaji  na  kitisho  cha  ugaidi."

Flüchtlingen im Mittelmeer
Wakimbizi wakisafirishwa baharini kwenda Ulaya kupitia bahari ya MediteraniaPicha: picture-alliance/dpa/A. Surinyach/AP

Makubaliano  na  Uturuki

Umoja  wa  Ulaya  unahaja  ya  kulinda  makubaliano  na  Uturuki ambayo  yametokana  na  wimbi  la  wahamiaji kupitia  ardhi  ya Uturuki la  watu  kutoka  katika  maeneo  ya  mizozo. Uturuki hapo nyuma  iliwahi  kuhoji  nia  thabiti  ya  Umoja  wa  Ulaya  ya kutekeleza  upande  wake  wa  makubaliano.

Mahusiano  kati  ya  Ankara  na  Umoja  wa  Ulaya  yameporomoka tangu  kushindwa  kwa  jaribio  la  mapinduzi  Julai  mwaka  2016 ambalo  lilifuatiwa  na  hatua  za  kukamatwa  kwa  maelfu ya  watu nchini  humo. Wakosoaji  wanamshutumu  rais Recep Tayyip Erdogan  kwa  kutumia  kisingizio  cha  mapinduzi  kuwabana wapinzani wa  kisiasa.

Litauen Vilnius - Interview mit Litauens Außenminister Linas Linkevicius
Waziri wa mambo ya kigeni wa Lithuania Linas LinkeviciusPicha: Außenministerium von Litauen/T. Razmus

Uturuki  ambayo  ilitia  saini  makubaliano  ya  ushirika  na  Umoja wa  ulaya  mwaka  1963, ilianza majadiliano  rasmi ya  kujiunga  na Umoja  huo  mwaka  2005. Hata  hivyo , wanachama  kadhaa , ikiwa ni  pamoja  na  Ufaransa , wamepinga  mazungumzo  hayo  ama baadhi  ya  vipengee ikiwa  na  maana  kwamba  ni  sura 16 tu za majadiliano  kati  ya  35 zimekwisha  funguliwa.

Mawaziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Finland  na Lithuania wamezungumzia  pia  dhidi  ya  kutovunja  mazungumzo  na  Uturuki.

"Hapana, tunapaswa  kuendelea  na  mchakato wa mahusiano. sio rahisi  lakini  tunapaswa  kuthamini  mahusiano," waziri  wa  mambo ya  kigeni  wa  Lithuania Linas Linkevicius  amewaambia  waandishi habari.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Yusuf Saumu