Macron azungumzia suala la haki za binadamu na Al Sisi
28 Januari 2019Muda mfupi baada ya kuwasili nchini Misri siku ya Jumapili katika ziara yake ya siku tatu nchini humo, Macron alisema anatarajia kuwa na majadiliano ya kweli na Rais Sisi juu ya haki za binaadamu. Macron amesema mambo nchini humo yamekuwa mabaya zaidi tangu rais Abdel Fatah Al sisi alipoutembelea mji wa Paris mwaka 2017.
Amesema mpaka sasa bado wapinzani wanaendelea kuwepo korokoroni pamoja na waandishi habari na wanablogu jambo ambalo ni tishio kwa uthabiti wa nchi.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari mjini Cairo, Macron amesema anachokisimamia ni uthabiti na uhuru wa dola lakini kile kinachoendelea nchini Misri ikija katika masuala ya haki za binaadamu ni jambo linalotishia uthabiti huo.
"Uthabiti na amani ya muda mrefu vinaendana pamoja na heshima ya haki ya utu na utawala wa sheria na katika kutafuta uthabiti hakuwezi kutenganishwa na masuala ya haki za binaadamu," alisema rais Macron.
Ufaransa ambayo inajitambua kama taifa ambalo ni chimbuko la haki za binaadamu imekuwa ikishinikizwa kuwa na mazungumzo na Jenerali aliegeuka kuwa rais Abdel Fattah al sisi ambapo rikodi yake ya haki za binaadamu inakosolewa kwa kiwango kikubwa na kuonekana kuwa mbaya zaidi kila kukicha.
Serikali ya Al Sisi inaonekana kuwa ya misimamo mikali kuliko serikali ya kiongozi wa zamani Hosni Mubarak
Serikali ya Sisi inaangaliwa na mashirika ya kiraia nchini humo kuwa na misimamo mikali kuliko serikali ya Hosni Mubarak rais wa muda mrefu aliyeondolewa mwaka 2011.
Hata hivyo Rais Abdel Fattah al Sisi amewaambia waandishi habari kwamba haki za binaadamu zizingatiwe kwa kuangalia muktadha wa machafuko yaliomo katika eneo hilo katika vita dhidi ya ugaidi. Amesema Misri haijengwi na wanablogu bali inaendelea na kujengwa kupitia ajira, juhudi na kuvumiliana kwa watu wake.
Awali Macron alitupilia mbali pendekezo kwamba silaha kutoka Ufaransa zinatumiwa dhidi ya watu wa Misri akisema silaha hizo zimetumika tu katika operesheni za kijeshi. Rais huyo wa Ufaransa ameongeza kuwa hakuna mikataba yoyote mipya ya kijeshi iliozungumziwa katika mkutano wake na Al sisi kando na mpango wa kutoa ndege 12 za kivita kwa Misri.
Sisi na Macron wametia saini mipango ya kiuchumi na kimaendeleo ikiwemo usaidizi wa Ufaransa katika masuala ya sera za kijamii na biashara zitakazoendeshwa na wanawake na makubaliano ya kupanua sekta ya usafiri nchini Misri.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo