1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na jinsi anavyoufatilia uchaguzi wa Ujerumani

9 Septemba 2021

Kitendo cha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kukutana na wagombea wawili wa nafasi ya ukansela Ujerumani kumrithi Angela Merkel kimeonesha jinsi Ufaransa inavyoufatilia kwa karibu uchaguzi huo utakaofanyika Septemba 26.

https://p.dw.com/p/406vJ
Paris Frankreich Präsident Emmanuel Macron Pressekonferenz
Picha: Sebadelha Julie/Abaca/picture alliance

Siku ya Jumatatu Rais Macron alikutana na Olaf Scholz, Waziri wa Fedha wa Ujerumani na Makamu Kansela wa chama cha mrengo wa kushoto cha Social Democratic, SPD ambaye anaongoza katika utafiti wa maoni na Jumatano alikutana na Armin Laschet kutoka chama cha Merkel cha Christian Democratic Union, CDU.

Huku mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Ikulu Elysee yakiwa ya faragha bila kutolewa taarifa kwa waandishi habari, mikutano yote imesababisha uvumi mkubwa nchini Ujerumani kuhusu nani huenda Ufaransa inamuunga mkono au inatabiri atashinda.

Macron alimkaribisha Scholz kwa siku mbili kabla ya kukutana na Laschet mrithi wa Merkel, huku akiwa hajafanya mkutano wowote na mgombea wa ukansela kupitia chama cha Kijani, Annalena Baerbock, ambaye wakati mmoja alionekana kama anaweza kuwa kansela ajaye wa Ujerumani.

BM Scholz trifft Emmanuel Macron in Paris
Olaf Scholz na Rais Emmanuel MacronPicha: Thomas Imo/photothek.net/picture alliance

Gazeti la Die Welt limeripoti kuwa ziara za wagombea hao wawili wa SPD na CDU zinaipa kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani mwelekeo usio wa kawaida wa Ulaya. Ukweli kwamba Scholz alikuwa wa kwanza kukaribishwa na Macron huenda ikawa ni bahati tu, hata kama wachambuzi wa kisiasa wataona kama ni ishara ya siri ya upendeleo.

Baada ya mazungumzo yake ya Macron, Scholz aliitaja Ufaransa kama mshirika muhimu wa Ujerumani katika kuimarisha uhuru wa Ulaya kwenye ulimwengu unaobadilika. Huku Macron akifurahia uhusiano wake na Merkel, wakati mwingine kulikuwa na mivutano kuhusu ugumu wa bajeti ya Ujerumani, na Ufaransa inatarajia kuwepo njia rahisi zaidi ikiwa Scholz atashinda na kuwa kansela wa Ujerumani.

Scholz na anachotaka kukifanya

Gazeti la kila siku la Ufaransa, Le Monde limeandika kuwa Scholz ameiashiria Ufaransa kile anachotaka kukifanya kama kansela na kile ambacho ameshindwa kufanya kama makamu kansela.

Katika ziara ya jana, Laschet alitoa wito wa kuwepo ushirikiano imara kati ya Ufaransa na Ujerumani katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Huku kesi ya watuhumiwa wa mashambulizi ya Paris yaliyofanyika mwaka 2015 ikiwa imeanza kusikilizwa jana Jumatano, Laschet alitolea mfano wa sehemu ambayo Ujerumani na Ufaransa zinaweza kuanzisha mpango mpya wa Ulaya. ''Mashambulizi haya yameonesha suluhisho la Ulaya pekee ndiyo linatufanya tuwe na nguvu katika mapambano dhidi ya ugaidi. Tunatakiwa tuwe na polisi ya Ulaya kama ilivyo kwa FBI ya Marekani,'' alifafanua Laschet.

Frankreich | Treffen Armin Laschet mit Präsident Emmanuel Macron
Armin Laschet mgombea ukansela wa chama cha CDUPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Mgombea huyo wa ukansela kwa tiketi ya CDU amebainisha kuwa washambuliaji hao waliingia kutoka Brussels na kusafiri kupitia Ujerumani, kabla ya kuishambulia Paris. Laschet, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa jimbo la North Rhine-Westphalia amesema Macron hajaonyesha matarajio yoyote madhubuti kuhusu ushiriki wa jeshi wa Ujerumani katika mipango ya kiulinzi ya Ulaya. Hata hivyo, amesema lazima wawe tayari kutoa mchango wao katika sera ya ulinzi ya Ulaya.

Akiizungumzia hali ya Afghanistan, Laschet amesema Ulaya inapaswa kuwa na mamlaka katika sera yake ya kigeni na ulinzi. Amesema wao kama watu wa Ulaya pia wanapaswa kuwa na uwezo wa kuchukua hatua katika maeneo ambayo Marekani haiwezi. Ametoa wito wa kuwepo kwa sera ya kawaida ya kigeni ya Umoja wa Ulaya na maamuzi mengi na miradi ya pamoja ya silaha kwa ajili ya kuokoa pesa na kwa ufanisi zaidi wakati wanapotoa vifaa.

Macron anayeonekana kama mwanasiasa mwenye nguvu zaidi katika Umoja wa Ulaya baada ya Merkel kuondoka, anataka kuutumia urais wake kushinikiza ajenda kabambe ya kiuchumi na uhuru wa kimkakati kuifanya Ulaya isiwe tegemezi sana kwa Marekani. 
 

(DPA, AFP)