Macron na Le Pen kupambana duru ya pili
24 Aprili 2017Kwa mujibu wa matokeo ya kura, Macron amepata asilimia 23.9 ya kura na Le Pen amepata asilimia 21.4. Kura za maoni zilizochapishwa hapo jana zinaonyesha kwamba Macron atamshinda Le Pen kwa urahisi katika duru ya pili. Akihutubia baada ya ushindi wake hapo jana Macron alisema. Macron alisema tangu kuundwa kwa Jumuiya yake ya kisiasa mwaka mmoja uliopita, siasa za Ufaransa zimebadilika. Kiongozi huyo amesema anataka kuwa rais atakae wawezesha watu wanaotaka kuwa wabunifu na wenye ari ya kutenda kazi ili kuyafikia malengo yao kwa urahisi na haraka zaidi. Mgombea mwingine aliyefanikiwa kuingia katika raundi ya pili ya uchaguzi kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen amewataka Wafaransa waitumie fursa ya kihistoria iliyopo. Le Pen amesema wakati umefika wa kuwakomboa Wafaransa kuondokana na kiburi cha tabaka la watawala. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa na mashirika ya IPSOS na HARRIS baada ya matokeo ya duru ya kwanza iliyofanyika jana Jumapili, asilimia kati ya 62 na 64 ya wapiga kura watapendelea Macron ashinde katika duru ya pili.
Mgombea wa chama cha kisoshalisti Benoit Hamon, Waziri mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve na mgombea urais wa chama cha kihafidhina Francois Fillon walioshindwa, wametoa mwito kwa wapiga kura wa kumuunga mkono Macron katika uchaguzi wa duru ya pili.
Juu ya ushindi wa Emmanuel Macron katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye yuko ziarani nchini Jordan amempongeza Emmanuel Macrfon kwa ushindi wake. Bwana gabriel amesema anamini kuwa inapasa kusema uchaguzi huo unatoa fursa kubwa barani Ulaya. Emmanuel Macron atakuwa rais wa Ufaransa atakae wakilisha mwanzo mpya barani Ulaya, ambaye hataridhika na hali ya mkwamo ambayo wakati mwingine huoenekana barai humu. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ameongeza kusema Macron pia atazileta Ujerumani na Ufaransa ili zikaribiane zaidi.
Ufaransa sasa inakabiliwa na mvutano kati ya pande mbili baina ya Macron anayetetea sera ya kuwepo kwa Umoja wa Ulaya na katika upande mwingine Marine Le pen anayepinga uhamiaji na ambaye ameahidi kufanyika kura ya maoni juu ya Ufaransa kuendelea kuwamo au kujiondoa Umoja wa Ulaya. Le Pen amesema sasa utafanyika mjadala mkubwa na raia wa Ufaransa wataamua kati ya sera ya dunia utandawazi inayotekelezwa kwa kasi na Ufaransa yenye mipaka imara. Duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini Ufaransa itafanyika tarehe 7 mwezi ujao ambapo Wafaransa watamchagua kiongozi wao mpya.
Mwandishi; Zainab Aziz/DPAE/RTRE
Mhariri:Caro Robi