Macron: Wanawake wameathirika zaidi na COVID-19
1 Julai 2021Akiufungua mkutano huo ulioandaliwa na Ufaransa na Mexico siku ya Jumatano, Rais Macron amesema wanawake mbali na kuwa waathirika wa kwanza, wamekumbana na unyanyasaji wa kijinsia ambao umeongezeka hasa katika wakati wa kuweka vizuizi vya kukabiliana na janga la COVID-19.
"Wakati walikuwa mstari wa mbele kupambana na COVID-19, wanawake wamekuwa waathirika wa kwanza katika mzozo huu wa kiafya. Pia tunajua kwenye nchi zetu ikiwemo Ufaransa, hatua zilizowekwa kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, unyanyasaji dhidi ya wanawake uliongezeka tena," alisema Macron.
Macron pia alithibitisha kuhusu "uhafidhina mpya" ambao unazishambulia haki za wanawake.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alibainisha kuwa suala la usawa bado halijapewa uzito. Merkel amesema Ujerumani itawekeza euro milioni 140 zaidi, katika kutekeleza haki ya kiuchumi na kuifanya nchi hiyo kuchangia euro milioni 240.
Merkel amesema pesa hizo ni uwekezaji ambao utawanufaisha wasichana hasa katika elimu pamoja na kuwepo mazingira mazuri ya kazi na kuimarisha haki ya wanawake kumiliki mali.
Clinton na yaliyojiri Beijing
Wakati huo huo, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton amekumbushia kuhusu mkutano wa wanawake uliofanyika mwaka 1995 mjini Beijing, China. Wakati huo, mkutano uliorodhesha madai ambayo yalipitishwa na nchi 189 yenye lengo la kufanikisha usawa wa kijinsia katika maeneo yote kwenye jamii.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris alionya kuwa demokrasia iko hatarini ulimwenguni kote na kwamba usawa wa kijinsia unaimarisha demokrasia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wanawake, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema wanawake ulimwenguni wamebanwa kwenye kona ndogo.
"Kuna robo moja tu ya wanawake ambao ni mameneja. Na robo moja ya wabunge duniani. Robo moja ni wale wanaochangia mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi. Chini ya robo moja ni wale wanaojadili makubaliano ya amani. Na maamuzi yote haya yana athari kubwa katika uwezo wao wa kuwa na maisha yenye maana," alifafanua Phumzile.
Ahadi ya dola bilioni 40
Aidha, katika mkutano huo Wakfu wa Bill na Melinda Gates umeahidi kuchangia dola bilioni 40 kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na wasichana. Wakfu huo tayari unachangia dola bilioni 2.1 kupambana na ubaguzi, huku nyingi ya pesa hizo zikitumika katika afya na uzazi wa mpango katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Viongozi wengi na wakuu wa nchi walihudhuria ufunguzi wa mkutano huo kuhusu usawa wa kijinsia, akiwemo Rais wa Halmashari Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambaye alisema kuwa uchumi wa kwenye mtandao bado unadhibitiwa na wanaume.
(DPA, AP)