1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari Kenya wapewa siku 5 waache kugoma

26 Januari 2017

Mahakama ya Kenya siku ya Alhamisi (26.01.2017) imewapa madaktari na wauguzi siku 5 kumaliza mgomo wao. Hatua hiyo inabadili msimamo wa awali wa serikali kutishia kuwatupa gerezani maafisa wa chama cha madaktari.

https://p.dw.com/p/2WSXp
Kenia Narobi Ärztestreik
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mgomo huo ulioanza Desemba 5 mwaka uliopita umesababisha hospitali za umma kufungwa na wagonjwa kukosa huduma za kimsingi za matibabu kwa zaidi ya wiki saba. Hellen Wasilwa, jaji wa mahakama ya Kenya inayohusika na mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi, alipitisha hukumu ya kifungo cha mwezi mmoja mnamo Januari 12 mwaka huu dhidi ya maafisa wa chama cha madaktari ambayo haijaanza kutekelezwa na kuwaamuru waukomeshe mgomo huo katika kipindi cha wiki mbili.

Lakini muda huo ulipopita siku ya Alhamisi jaji Wasilwa aliwapa maafisa hao siku nyingine tano kufanya hivyo. "Naahirisha hukumu kwa siku nyingine tano na muda huu sio wa kufanya mashauriano bali ni wa wao kuagiza mgomo ukome," alisema jaji Wasilwa. Maafisa wa chama cha madaktari wanatakiwa kufika mahakamani Januari 31.

Madaktari wamekataa pendekezo la serikali kuwapa nyongeza ya mshahara ya asilimia 40 wakisema ni kidogo na inavunja ahadi zilizotolewa katika makubaliano ya mwaka 2013 na haitilii maanani masuala mengine kama vile uhaba wa wafanyakazi na ukosefu wa vifaa.

Madaktari wasema hawabanduki

Madaktari wanasisitiza kwamba haja yao si nyongeza ya mishahara bali kutekelezwa kwa mkataba uliotiwa saini kati yao na serikali miaka mitatu iliyopita.

Kenia Kenyatta National Hospital - Krankenhaus in Nairobi
Picha: picture-alliance/dpa/Kenyatta National Hospital

Profesa Elija Ogola, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi anayefunza taaluma ya udaktari alisema, "Tungependa kuunga mkono msimamo wa Muungano ambao ni msimamo wa madaktari kwamba suala la majadiliano sio kuongezwa kwa mishahara wala marupurupu bali kutekelezwa kwa mkataba wa makubaliano".

Mgomo huo ambao uliingia siku ya yake ya 50 Alhamisi umesababisha maafa katika hospitali za umma huku wagonjwa wengi wakisongamana katika hospitali za kibinafsi.

Mgomo huo unafanyika wakati ambapo kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017 zimepamba moto huku upinzani ukiutumia kama silaha ya kuitandika serikali. Serikali kwa upande wake haijatoa mwelekeo wa kudumu kuhusiana na mgomo huo mbali na kuwatisha madaktari kuwaachisha kazi. Madaktari nao wametisha kustaafu kwa pamoja jambo ambalo huenda likalemaza sekta nzima ya afya. Zaidi ya madaktari 500 pamoja wahadhiri wa vyuo vikuu wanashiriki mgomo huo ulioanza mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka uliopita.

Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini Kenya pia walianza mgomo wiki moja iliyopita wakidai nyongeza ya mshahara. Migomo hiyo inayovuruga shughuli muhimu nchini humo inafanyika kabla uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

MwandishI: Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdulrahman