Madaktari wakaidi amri ya mahakama na kuendelea kugoma Kenya
15 Machi 2024Mgomo huo wa madaktari ulioanza saa chache zilizopita, umezorotesha utoaji wa huduma katika hospitali za umma. Frederick Goli alihitaji matibabu kwasababu ya tatizo la mguu baada ya kufanyiwa upasuaji, kwenye hospitali ya mafunzo na rufaa ya Kakamega na analalamika hakuhudumiwa. "Nilikuwa nimepewa miadi ya Asubuhi, kwa daktari wa mifupa, kwasababu nilifanyiwa upasuaji, nimefika hospitali tumeambiwa wamegoma." alisema bwana Goli.
Pauline Wanjiru alihitaji huduma baada ya mwanawe kuvunjika mguu na sasa hali yake inaendelea kuwa mbaya na anachelea kurejea nyumbani. "Sijapata daktari, siku nyengine tulikuwa tunatibiwa vizuri lakini sasa hatutibiwi na kijana wangu alivunjika mguu na huo mguu unaanza kuoza," alisema Pauline Wanjiru.
Jaji Byrum Ongaya anatazamiwa kutoa mwelekeo baada ya uongozi wa hospitali kuu ya Kenyatta kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mgomo huo wa madaktari kwa madai kuwa wagonjwa watataabika. Jaji Ongaya alimuamuru siku ya Jumatano waziri wa masawala ya ajira Florence Bore kuandaa kikao cha pande tatu kitakachowaleta pamoja madaktari, viongozi wa muungano wao wa KMPDU na waajiri wa umma.
Madaktari wa Nairobi waanza mgomo
Ajenda ilitakiwa kujikita katika kusaka suluhu ya minunguniko na malalamiko ya madaktari kama iliyoelezea ilani ya mgomo.Hata hivyo msimamo wa madaktari ni kuwa hawajasikilizwa. Dr Aggrey Orwenyo ni katibu mkuu wa chama cha madaktari, KMPDU tawi la Kisii na amesema msimamo wao uko pale pale.
Baadhi ya madaktari hawakubaliani na mgomo unaoendelea
Kwa upande wa pili , baadhi madaktari wana mtazamo tofauti kuhusu mgomo huo wa kitaifa.Dr Ahmad Mkuche anayehudumu kwenye hospitali ya Samburu iliyoko kaunti ya Kwale anabainisha kuwa kususia kazi sio suluhu.
Miezi mitatu ya mgomo wa wauguzi Kenya
Kikao kilichotarajiwa cha pande tatu kinalenga kuepusha maafa kabla ya suluhu ya kudumu kupatikana.Dr Tom Nyamwira ni mkuu w autoaji huduma kwenye hospitali ya rufaa ya Kisumu na anaeleza kuwa wanajitahidi.
Kwa upande wao, madaktari wanaishinikiza serikali kutenga asilimia 15 ya bajeti ya taifa kwa masuala ya afya. Kwa mujibu wa katibu mkuu wa chama cha madaktari KMPDU, Dr Davji Atellah,msimamo wao ni kwamba hawatarejea kazini hadi wasikilizwe na suluhu ipatikane. Serikali inashikilia haina hela za kugharamia mchakato huo.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya