1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari wa Ujerumani waruhusiwa kumuona Navalny

21 Agosti 2020

Madaktari wa Ujerumani waliokwenda Siberia kwa nia ya kumsafirisha mwanasiasa wa upinzani ambaye ni mkosoaji wa Rais wa Urusi Vladmir Putin, Alexei Navalny waruhisiwa kumuona katika hospitali alikolazwa ya Omsk.

https://p.dw.com/p/3hJSY
Russland Vergiftung Navalny Krankentransport nach Deutschland
Picha: Reuters/A. Malgavko

Madaktari wa Ujerumani waliokwenda Siberia kwa nia ya kumsafirisha mwanasiasa wa upinzani ambaye ni mkosoaji mkubwa wa rais wa Urusi Vladmir Putin, Alexei Navalny wameruhisiwa kumuona siku ya Ijumaa katika hospitali alikolazwa ya Omsk. Lakini pia Ujerumani ilitowa tamko hapo awali ikisema maisha ya mwanasiasa huyo yanapaswa kuokolewa.

Kuruhusiwa kwa timu ya madaktari wa kijerumani kumuona Navalny kumetejwa na msaidizi wake kuwa ni hatua nzuri. Leonid Volkov msaidizi mwandamizi wa mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Urusi ndiye aliyetowa taarifa hiyo kwa waandishi habari akiwa mjini Berlin nchini Ujerumani. Madaktari wa Kijerumani walisafiri kuelekea Siberia kwa kutumia ndege maalum ya huduma za matibabu ya shirika lisilo la kiserikali, kwa lengo la kwenda kumchukua Alexei Navalny aliyeko katika hali mahututi na waliwasili jana alhamisi usiku. Lakini madaktari wanaomtibu wameshasema leo kwamba hayuko katika hali ya kuweza kusafirishwa.

Alexej Navalny
Alexei NavalnyPicha: Imago Images/Itar-Tass/S. Fadeichev

Taarifa pia zinaelezwa kwamba mke wa mwanasiasa huyo Yulia Navalnaya ameandika barua ya kumuomba rais Vladmir Putin aruhusu mumewe asafirishwe Ujerumani kwenda kutibiwa akisema anaamini anahitaji huduma ya matibabu ya madaktari bingwa nchini Ujerumani.

Lakini kwa upande mwingine pia msaidizi mwandamizi wa Navalny amesisitiza kwamba familia ya mwanaharakati huyo bado haijapewa majibu yoyote ya vipimo na wala ripoti ya uchunguzi na wala hawajapata data za kuaminika kuhusu hali yake,huku akiwashutumu maafisa wa Urusi kwa kujaribu kuendesha mikakati ya hila za kuuzima ukweli. Amewaomba viongozi wa Umoja wa Ulaya kusaidia kushinikiza Navalny asafirishwe.

Washirika wa Navalny wanawataka madaktari wakijerumani kumsafirisha akatibiwe nchini Ujerumani mwanasiasa huyo, lakini madaktari wa Urusi katika hospitali hiyo ya Omsk wanasema hali yake sio thabiti ya kumuwezesha kusafiri. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert hata hivyo amesema daktari wa Navalny atapelekwa kutathmini hali ya mpinzani huyo wa Putin kuona ikiwa anaweza kusafirishwa. Aidha serikali ya Ujerumani imeyapokea madai mazito kwamba Navalny alipewa sumu na kutaka uchunguzi makini na wa kina ufanyike, ingawa madaktari wa Urusi wamedai hakuna ushahidi wa hilo.

Russland Omsk | Alexander Murachowski - Leitender Arzt des City Clinical Emergency Hospital
Daktari mkuu wa Urusi, Alexander MurakhovskyPicha: picture-alliance/dpa/A. Kryazhev

Madaktari wa Urusi wakiongozwa na daktari mkuu Alexander Murakhovsky wanaamini mwanaharakati huyo alipoteza fahamu na kufikia hali ya kuwa mahututi kwasababu ya kushuka ghafla kwa kiwango cha sukari kwenye damu, hali ambayo ilisababishwa na tatizo linalotokana na mvurugiko wa mfumo wa kemikali za mwili. Murakhovsky amewaambia waandishi habari kwamba masuali mengi ya kisheria yatabidi kutatuliwa kabla ya Navalny kukabidhiwa kwa madaktari wa Ulaya.

Kadhalika madaktari wa hospitali hiyo ya Omsk iliyoko kwenye jimbo la Siberia wamesema hali ya Navalny imeimarika kiasi usiku lakini maisha yake bado yako hatarini.Kwa upande mwingine naibu waziri wa ufaransa anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Clement Beaune amesema nae pia anawasiwasi na hofu kuhusu hatma ya mwanaharakati huyo wa siasa za upinzani na akasisitiza kwamba Ufaransa iko tayari kumsaidia ikiwa itahitajika.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW