1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madhila wanayopitia watoto wakimbizi wanaowasili Uganda

Lubega Emmanuel 22 Julai 2020

Huku Uganda ikiendelea kuwapokea wakimbizi kutoka mataifa jirani ya DRC na Sudan Kusini, mashirika ya kuwahudumia wakimbizi yanakabiliwa na changamoto ya kuwashughulikia watoto wasioandamani na wazazi.

https://p.dw.com/p/3fgOL
Flüchtlinge Sudan  Südsudan
Picha: picture-alliance/dpa/B. Curtis

Wengi wa watoto hao ni wale ambao wazazi wao wameuawa katika mapigano au kupoteana nao katika sintofahamu inayozuka kufuatia mashambulizi ya makundi ya wapiganaji katika nchi hizo.

Kulingana na takwimu za shirika la Umoja Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR, zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi wanaopokelewa Uganda ni watoto. Mamia miongoni mwa hao ni wale ambao hawakuandamana na wazazi au jamaa zao wa karibu.

Mchakato wa kuwachuja watoto wakimbizi ambao hawakuandamana na wazazi wao huanza mara tu wanaposajiliwa baada ya kuvuka mpaka. Wale ambao wameandamana na jamaa zao hutengwa lakini hufuatiliwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma na malezi mazuri. Kundi la wale ambao hawana mtu yeyote waliyeandamana naye hushughulikiwa kwa kukabidhiwa familia za wanaojitolea kuwapa malezi.

Uganda Flüchtlingslager Palorinya Südsudan
Wakimbizi wa kutoka Sudan Kusini wakiwasili kambi ya Palorinya Picha: DW/L. Emmanuel

Chantal Munyandinda ni mmoja kati ya akina mama waliojitolea kuwalea watoto wakimbizi ambao hawana jamaa zao. Anamlea msichana wa umri wa miaka 12 huku shirika la msalaba mwekundu likiendelea kuwatafuta wazazi na jamaa za mtoto huyo.Yeye mwenyewe alikuwa kama watoto hao mwaka wa 2009 wakati alipopoteana na wazazi wake kufuatia mapigano nchini kwao DRC.

Lakini watoto wakimbizi waliotimu umri wa kati ya miaka 14 hadi 17 wana chaguo la kuishi pekee yao bila kukabidhiwa familia yoyote. Wengine kati yao huamua kuwalea wadogo zao badala ya kutunzwa katika familia zingine. Hata hivyo, kundi aina hili huhitaji kupewa nasaha na mwongozo kila mara katika umri wao wa ujana la sivyo wanaweza kushawishika kushiriki maovu na uhalifu mbalimbali au hata kufanyiwa manyanyaso yanayokiuka haki zao kama watoto.

Katika mataifa mengine watoto wa aina hii wangewekwa katika makao ya kuwatunza watoto. Lakini,wanajamii pamoja na wadau katika kuwatunza watoto wakimbizi wanakubaliana kuwa jadi na utamaduni wa Kiafrika kwamba malezi ya mtoto ni jukumu la kila mtu ndiyo vizingatiwe kuhusiana na malezi ya watoto hao.

Hata hivyo, baadhi ya watoto wanaelezea kuishi maisha ya kubaguliwa na kunyanyaswa na familia walizokabidhiwa na ndiyo maana wengine hutoroka kutoka familia hizo. Chantal Munyandinda yeye alibahatika kukutanishwa na wazazi wake baada ya miaka miwili.

Angalau kuna watoto waliopoteleana au kuwapoteza wazazi wao wanaobahatika kukutanishwa kwao huku wengine wakitunzwa vyema na familia walizokabidhiwa hadi wanapofikia umri wa kujitegemea wenyewe. Kulingana na tawkimu za UNHCR nchini Uganda kuna zaidi ya watoto wakimbizi 42,000 ambao wanatunzwa na familia za watu ambao si jamaa zao katika kambi na makao ya wakimbizi.