Maelfu waandamana Mali kuunga mkono jeshi na kupinga vikwazo
15 Januari 2022Maandamano hayo yaliandaliwa na kuratibiwa na watawala wa kijeshi, kama mbinu ya waziri mkuu wa mpito Choguel Maiga kutuma ujumbe kwa mataifa yaliyoiwekea vikwazo serikali yake.
Wiki iliyopita, wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS waliiwekea vikwazo vikali Mali, baada ya watawala wa kijeshi wa nchi hiyo kuahirisha uchaguzi uliopngwa kufanyika Februari mwaka huu na kuuhamishia Desemba 2025.
Soma zaidi:Urusi,China zazuia juhudi za kuunga mkono vikwazo kwa Mali
Kulingana na mwandishi wa DW nchini Mali, ni mara chache sana kwa waandamanaji kukusanyika katika uwanja wa Uhuru mjini Bamako, ulikojumuika umati mkubwa waandamanaji.
"Ungana kama mtu mmoja"
Jukwaa kubwa lilijengwa katikati ya mnara wa ukumbusho wa Uhuru ili kukaribisha hotuba za Imam Oumarou Diarra, waziri wa serikali ya Choguel Maiga, ambaye alifanya mahubiri ya Ijumaa kwa waumini wa Kiislamu.
Waandamanaji kadhaa walijipamba kwa rangi za bendera ya taifa ya Mali. Dalili za chuki dhidi ya Ufaransa na ECOWAS na kupendelea ushirikiano kati ya Mali na Urusi pia zilikuwepo, kama vile mabango yenye picha ya Kanali Assimi Goita na mamlaka ya mpito ya Mali.
Soma zaidi: Wito wa maandamano kupinga vikwazo vya ECOWAS nchini Mali
Wanawake hawakubaki nyuma katika uhamasishaji huu wa kukemea vikwazo. Wengi wao walishiriki maandamano wakivalia vitambaa vyeupe ambalo ni vazi la kitamaduni.
Mwishowe, ilikuwa hali ya sherehe iliyoshamiri sauti za vuvuzela ambazo zilihanikiza kila mahali mjini Bamako.
Mwandamanaji mmoja alisema, "watu wa Mali lazima wajipange na kuungana kama kitu kimoja kumuunga mkono kiongozi wao Kanali Assimi Goïta, ambaye alithubutu kupinga ubeberu wa Ufaransa."
Shinikizo la kimataifa
Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa Mali pamoja na nchi nyingi katika jumuiya ya ECOWAS imeunga mkono dhidi ya Mali. Umoja wa Ulaya na Marekani pia zimekaribisha vikwazo hivyo na shinikizo dhidi ya wanajeshi walionyakua madaraka.
Maandamano yalifanyika mbele ya Ubalozi wa Ufaransa mjini Bamako, ambao ulinzi wake ulikuwa umeimarishwa, na pia katika miji mingine mikubwa ya Mali, kama vile Timbuktu na Mopti.
Soma zaidi: ECOWAS yafunga mipaka yake na Mali
Mbali na waziri mkuu na mawaziri wake, viongozi wengine waandamizi walishiriki katika maandamano haya, na walishangiliwa na waandamanaji kila walipopita.
Vyanzo: afpe, ape