1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Siku ya Wafanyakazi Duniani

1 Mei 2016

Mei Mosi ni siku ya wafanyakazi ya kimataifa ambapo vyama vya wafanyakazi huandamana duniani kote kupigania haki za wafanyakazi wenye kukabiliwa na ukosefu wa ajira unaochochea hasira dhidi ya serikali.

https://p.dw.com/p/1IgAJ
Picha: Getty Images/A. Koerner

Maelfu ya watu katika miji ya Berlin na Hamburg nchini Ujerumani wameshiriki maandamano ya kuadhimisha siku hiyo ya wafanyakazi ambapo kwa kiasi fulani maandamano hayo yamefanyika kwa amani huku polisi ikiripoti baadhi ya matukio madogo ya vurugu.

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Ujerumani (DGB) limelani chuki dhidi ya wageni na sera kali za mrengo wa kulia katika maandamano yaliofanyika katika mji wa kusini magharibi wa Stuttgart Jumapili (01.05.2016).

Kiongozi wa shirikisho hilo Reiner Hoffman amesema " madai ya wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia hayahusiani kabisa na mtengamano katika jamii,haki ya kijamii,utandawazi wenye kuzingatia haki au mshikamano". Kiongozi huyo alikuwa akimaanisha chama Mbadala kwa Ujerumani AfD ambacho kinafanya mkutano wake mkuu katika mji huo.

Hususan ameshutumu propaganda ya chama hicho dhidi ya wakimbizi.Shirikisho hilo pia limekosowa waajiri kwa kujinufaisha na mikataba ya kazi ya muda.

Maadhimisho Ujerumani yalikuwa tulivu

Msemaji wa polisi mjini Berlin amesema zilikuwa sherehe zisizokuwa na matukio makubwa ya vurugu ambapo hapo Jumamosi waandamanaji 2,300 waliingia mitaani kupinga kuongezeka kwa kodi za nyumba katika mji mkuu huo.

Mwenyekiti wa chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) Frauke Petry akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho Stuttgart. (01.05.2016)
Mwenyekiti wa chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) Frauke Petry akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho Stuttgart. (01.05.2016)Picha: Reuters/W. Rattay

Kwa mujibu wa polisi mjini Hamburg maandamano ya wafuasi wa sera za mrengo wa kushoto kwa kiasi kikubwa yalifanyika kwa amani, katika kisa kimoja polisi alijeruhiwa baada ya waandamanaji kuwarushia mawe na chupa. Waandamanaji pia walilitia moto gari moja la serikali.

Nchini Urusi katika mji mkuu wa Moscow maelfu wameandama katika uwanja wa Red Square wakati wa maandamano ya wafanyakazi yanayounga mkono serikali.

Kama iilivyo kwa maandamano yanayoandaliwa na chama cha United Russia ,maadamano ya Mei mosi hukwepa kumshutumu Rais Vladimir Putin au serikali yake kwa kupanda kwa gharama za maisha.Kauli mbiu zililenga mishahara na ajira kwa vijana waliosoma.

Vurugu Uturuki

Polisi ya Uturuki ilitumia gesi ya kutowa machozi kuwatawanya waandamanaji wa Mei mosi mjini Instambul.

Polisi wakipambana na waandamanaji Instambul(01.05.2016)
Polisi wakipambana na waandamanaji Instambul(01.05.2016)Picha: picture-alliance/dpa/T. Bozoglu

Purukushani ndogo zimetokea kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wakijaribu kwenda katika uwanja wa kihistoria wa Taksim ambao ni alama muhimu kama kituo cha maandamano yaliouwa watu 34 hapo mwaka 1977.Polisi 15,000 wamemwagwa mjini Istanbul.

Mjini Manila waandamanaji wapatao 2,000 wa sera za mrengo wa kushoto walipambana na polisi wa kuzuwiya fujo ambao walitumia ngao na maji ya kuwasha kujaribu kuwazuwiya waandamanaji waliokuwa wakipeperusha bendera kufika karibu na ubalozi wa Marekani.

Televisheni imeonyesha baadhi ya waandamanaji wakimtwanga makonde polisi mmoja aliyekuwa akirudi nyuma lakini hakuna mtu aliekamatwa.

Maadamano ya siku ya wafanyakazi yamefanyika nchini kote Ufilipino wakati kampeni zikiingia wiki ya mwisho kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa rais hapo Mei 9 ambapo baadhi ya wagombea wameahidi kushughulikia matatizo ya wafanyakazi.

Maduro apandisha mishahara

Rais anayepigwa vita wa Venezuela Nicolas Maduro ametangaza ongezeko la asilimia 30 ya kiwango cha chini cha mishahara licha ya nchi hiyo kuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.Picha: Reuters/M. Bello

Ongezeko hilo ambalo utekelezaji wake unanza Mei Mosi hii pia linakusudia kukabiliana na hali ya kupanda sana kwa gharama za maisha nchini humo ambapo kumeshuhudiwa kupandishwa mara kadhaa kwa mishahara ya kiwango cha chini na malipo ya uzeen katika miezi ya hivi karibuni.

Ufaransa ilikuwa katika hali ya tahadhari ya kiwango cha juu katika maadhimisho haya ya siku ya wafanyakazi duniani baada ya maandamano dhidi ya mipango ya mageuzi ya ajira wiki hii kugeuka ghasia kwa magari kutiwa moto na polisi kadhaa kujeruhiwa baada ya kupigwa mawe na waandamanaji.

Wakati serikali inataraji mageuzi hayo yatapunguza tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa asilimia 10 wakosoaji wanaamini yanatishia haki za wafanyakazi zilizopatikana kwa taabu kwa kufanya iwe rahisi kuwaachisha kazi waajiriwa wakati wa hali ngumu.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Walls ameonya Jumapili watakabiliana kwa nguvu kubwa na wale wenye kuleta fujo na kwamba kushambuliwa kwa vikosi vya usalama hakukubaliki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa/

Mhariri : Caro Robi