1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Warohingya wazuiliwa katika mpaka wa Bangladesh

31 Agosti 2017

Takriban Warohingya 27,000 ambao ni Waislamu, wamekimbia kutoka Myanmar na kuingia Bangladesh tangu Ijumaa wiki iliyopita. Wakati huohuo miili 20 ya Warohingya waliozama wakikimbia mapigano imepatikana.

https://p.dw.com/p/2j9uM
Bildergalerie Myanmar Rohingya Flüchtlinge flüchten nach Bangladesch
Picha: Reuters/M. Ponir Hossain

Walinzi wa mipaka nchini Bangladesh wamepata miili 20 ya wanawake na watoto wa jamii ya Rohingya, ambao boti yao ilizama walipokuwa wakitoroka machafuko ya Myanmar. Hayo yamesemwa na afisa mmoja wakati ambapo kukiwa na shinikizo kwa serikali mjini Dhaka kuwahifadhi maelfu ya watu wanaokimbia vita na ambao wamekwama mpakani.

Takriban Warohingya 27,000 ambao ni Waislamu, wamekimbia kutoka Myanmar na kuingia Bangladesh tangu Ijumaa wiki iliyopita. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vitatu kutoka Umoja wa Mataifa. Hali hiyo imejiri baada ya wanamgambo wa Rohingya waliojihami kwa visu na mabomu ya kienyeji kuvamia kituo cha polisi na kambi ya jeshi katika jimbo la Rakhine, hali iliyosababisha mapigano na watu 117 wakauawa.

Vijiji vyateketezwa

Warohingya wakibeba mali yao kukimbilia Bangladesh
Warohingya wakibeba mali yao kukimbilia BangladeshPicha: Reuters/M. Ponir Hossain

Ghasia hizo zinajiri wakati kukiwa na ripoti kuwa wanamgambo wa Kibudha wanateketeza vijiji vya Warohingya kwa moto. Noor Symon ambaye ni mmoja wa waathirika wa machafuko hayo anaelezea masaibu yanayowakumba huku akilia. "Wabudha wanatuua kwa risasi, wameteketeza nyumba zetu kwa moto na kujaribu kutupiga risasi, wameua mume wangu kwa risasi."

Duru za habari zimeeleza kuwa takriban Warohingya 20,000 wangali wamekwama mpakani kati ya nchi hizo mbili, huku chanzo kimoja cha habari kikisema idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi watu 30,000 jioni ya leo, kwani watu wanaendelea kukimbia vita hivyo vibaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita inayohusisha jamii hiyo ndogo ya Waislamu nchini Myanmar.

Myanmar imewaondoa maelfu ya Wabudha kutoka Rakhine kufuatia mapigano hayo ambamo wengi waliouawa ni wapiganaji wa jamii ya Warohingya na pia maafisa. Hayo ni kwa mujibu wa serikali ya Myanmar.

Changamoto kwa Aung San Suu Kyi

Watoto wa jamii ya Rohingya wakijaribu kuvuka mto kuelekea mpaka wa Bangladesh
Watoto wa jamii ya Rohingya wakijaribu kuvuka mto kuelekea mpaka wa Bangladesh Picha: Reuters/M. Ponir Hossain

Namna ya kuwahudumia takriban Warohingya milioni 1.1 nchini Myanmar ndiyo changamoto kubwa kwa kiongozi wa taifa hilo Aung San Suu Kyi ambaye amelaumiwa na wakosoaji wa kimagharibi kwa kutozungumza kwa niaba ya wachache ambao wamelalamikia kuuawa.

Alhamisi leo miili 11 ya watoto na 9 ya wanawake wote kutoka jamii ya Rohingya ilipatikana katika kingo za mto Naf baada ya boti yao kuzama walipokuwa wakikimbia machafuko.

Warohingya wamekuwa wakinyimwa haki za uraia nchini Myanmar na hivyo huchukuliwa kama wahamiaji haramu. Hii ni licha ya wao kudai kuwa chimbuko lao nchini humo ni tangu miaka na dahari.

Bangladesh yakataa kuwahifadhi

Mwnamke wa Rohingya alia huku amebeba mtoto baada ya kuzuiliwa na maafisa wa Bangladesh wanaolinda mpaka
Mwnamke wa Rohingya alia huku amebeba mtoto baada ya kuzuiliwa na maafisa wa Bangladesh wanaolinda mpakaPicha: Reuters/M. Ponir Hossain

Tangu miaka ya 1990, zaidi ya Warohingya 400,000 wamekuwa wakiishi katika mataifa maskini Kusini mwa Asia baada ya kukimbia kuuawa kutoka Myanmar.

Nayo bangladesh inaendelea kuwa katili dhidi ya Warohingya. Mnamo Jumatano, Bangladesh iliwarudisha Warohingya 366 waliokuwa wakijaribu kuingia nchini humo kutumia boti ndogo.

Shirika la kimataifa kuhusu uhamiaji limeungana na Umoja wa Mataifa kuisihi Bangladesh kuwapokea watu ambao wamekwama mipakani, lakini Bangladesh inasisitiza kuwa haina uwezo wa kutosha kuwakimu.

Mwandishi: John Juma/RTRE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga.