1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wasichana, wanawake walitekwa Msumbiji-Ripoti

Daniel Gakuba
7 Desemba 2021

Ripoti mpya ya Human Right Watch imesema kundi la kijihadi nchini Msumbiji, liliteka mamia ya wanawake na watoto katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado tangu mwaka 2018.

https://p.dw.com/p/43vQo
Mosambik | Provinz Nampula | Vertriebene Kinder Opfer von Terrorismus
Mashambulizi ya waasi kaskazini mwa Msumbiji yamesababisha madhila makubwa kwa raiaPicha: Roberto Paquete/DW

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu, limesema baadhi ya mateka hao wamekombolewa na vikosi vya serikali ya Msumbiji na washirika wa kikanda, lakini wengine bado hawajulikani walipo.

Kundi linalotuhumiwa kuufanya uhalifu huo linajulikana nchini Msumbiji kama Al Sunnah wa Jama'ah, au al-Shabab au Mashababos.

Soma zaidi: Mashambulizi ya magaidi wa Msumbiji kusini mwa Tanzania

Ripoti ya Human Rights Watch imesema kundi hilo la kijihadi liliwakamata kwa nguvu wanawake na wasichana walio na ngozi nyeupe nyeupe, na kuwalazimisha kuolewa na wapiganaji katika kile kinachoonekana kuwa ni utumwa wa kingono.

Wengine waliuzwa kwa wapiganaji wa kigeni kwa bei ya dola za Marekani kati ya 600 na 1200. Mateka ambao ni raia wa kigeni walifanikiwa kuachiwa huru baada ya familia zao kulipa fedha za kuwakomboa.

Mosambik | Muendumbe Cabo Delgado | Streitkräfte
Wanajeshi wa Msumbiji na washirika wa kikanda wamefanikiwa kuwakomboa baadhi ya wanawake waliochukuliwa matekaPicha: Roberto Paquete/DW

Rai ya kuachana na madhambi ya kingono

Mkurugenzi wa Human Rights Watch kwa ukanda wa Afrika, Mausi Segun, amesema amewataka viongozi wa kundi hilo la al-Shabab kuwaachia mara moja wanawake na wasichana wote linalowashikilia mateka, na kulihimiza kuchukua hatua zote zinazohitajika kuwakataza wapiganaji wao kujihusisha katika ubakaji na uhalifu mwingine wa kingono.

Amewataka pia kukomesha kuwaoza watoto, ndoa za kulazimisha na biashara ya kuwauza wanawake katika maeneo wanayoyadhibiti.

Kati ya Agosti 2019 na Oktoba 2021, Human Rights Watch ilifanya mahojiano na watu 37, wakiwemo mateka walioachiwa huru, jamaa wa mateka hao, maafisa wa usalama na viongozi wa serikali, na pia lilifuatilia ripoti katika vyombo vya habari kuhusu utekaji nyara huo.

 

Watoto wajiliwaza kwa sanaa Msumbiji

Vyanzo hivyo vililiarifu kuwa al-Shabab iliwachukuwa mateka wanawake na wasichana wakati wa mashambulizi yake katika wilaya kadhaa za jimbo la Cabo Delgado, kama Mocimboa da Praia mwezi Machi, Juni na Agost 2020, na Palma mnamo Machi mwaka huu wa 2021.

Alia na waasi wamchukue yeye, wamwache bintie

Mama mmoja wa miaka 33 alisema kundi hilo la waasi lilimkamata shangazi yake, na kumlazimisha chini ya mtutu wa bunduki kuwaonyesha nyumba zote walipo wasichana wa umri wa miaka kati ya 12 na 17 katika mji wa Diaca wilayani Macimboa da Praia.

Mama huyo anasema alihesabu wasichana 203, lakini hana uhakika ikiwa wote walichukuliwa mateka na al-Shabab.

Mosambik | Cabo Delgado Provinz
Nyumba na miundombinu vimeharibiwa katika vita jimboni Cabo DelgadoPicha: Marc Hoogsteyns/AP/picture alliance

Mwanamme wa miaka 27 alisema alimuona mama aliyekuwa akiwasihi waasi hao wamchukue yeye badala ya binti yake, lakini alijibiwa na mmoja wa wapiganaji kuwa hawawataki wanawake watu wazima, aliosema wana watoto na magonjwa.

Soma zaidi: Rwanda yakiri kupoteza askari wanne huko Cabo Delgado

Ripoti hii inabainisha kuwa mnamo miaka ya hivi karibuni serikali ya Msumbiji imefanikiwa kuwakomboa mamia ya mateka kutoka mikononi mwa waasi hao, lakini pindi wanaporejeshwa huzuiwa kwa wiki kadhaa bila mawasiliano na familia zao, katika kile kinachodhaniwa kuwa ni uchunguzi wa kiusalama.

 

Chanzo: Human Rights Report