Maelfu wahama makazi Somalia kutokana na mafuriko
13 Novemba 2023Waziri wa habari wa nchi hiyo Daud Aweis amesema watu takribani laki 500,000 wamehama makaazi yao kutokana mafuruko makubwa na kuonya kwamba wengine zaidi ya milioni moja huenda wakaathirika.
Waziri huyo ameongeza kwamba maafisa wa serikali wamethibitisha vifo vya watu 31 "lakini kuna uwezekano idadi ikaongezeka".
Uharibifu mkubwa umeshuhudiwa katika mkoa wa Gedo, ulioko kusini mwa Somalia pamoja na mkoa wa kati wa Hiran ambako kingo za Mto Shabelle zimevunjika na barabara kusombwa na maji katika mji wa Beledweyne.
Taifa hilo la pembe ya afrika limekumbwa na mvua kubwa isiyoisha tangu mwanzoni mwa mwezi huu kutokana na hali ya hewa ya El Nino.
Maafa hayo yanatokea baada ya kipindi kirefu cha ukame mkubwa ambao umesababisha kitisho cha baa la njaa kwa mamilioni ya Wasomali.
Somalia inachukuliwa kuwa moja ya nchi zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi lakini haina vifaa vya kutosha vya kukabiliana na maafa hayo, kwani kwa muda mrefu imekuwa ikipambana na uasi wa wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu.
Wiki iliyopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu, OCHA, lilisema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na "mafuriko makubwa katika karne" na kuonya kuwa watu milioni 1.6 wanaweza kuathirika.
Tahadhari ya UN: UN: Zaidi ya Wasomali 140,000 wakimbia makwako kutokana na msimu wa mvua za mafuriko
OCHA ilisema hali hiyo imechangiwa na athari za pamoja za matukio mawili ya hali ya hewa, El Nino na mfumo wa hali ya hewa katika bahari ya Hindi unaofafanuliwa na tofauti ya joto la juu ya bahari kati ya maeneo ya magharibi na mashariki mwa bahari.
El Nino kwa kawaida inahusishwa na ongezeko la joto duniani kote, pamoja na ukame katika baadhi ya maeneo ya dunia na mvua kubwa mahali pengine.
Kati ya Oktoba 1997 na Januari 1998, mafuriko makubwa yaliyosababishwa na El Nino yaliwaua watu zaidi ya 6,000 katika nchi tano za Pembe ya Afrika. Takriban watu 1,800 walifariki nchini Somalia ambapo kingo za Mto Juba ziliivunjika.
Soma pia: Mashirika ya UN yaonya kuhusu njaa kali Somalia
Kuanzia Oktoba hadi Novemba 2006, mafuriko yaliyosababishwa na mvua zisizo za msimu yaliwaua zaidi ya watu 140 huku wengi wakifa maji lakini wengine wakiuawa na mamba au kukumbwa na janga la malaria.
Mwishoni mwa mwaka wa 2019, takriban watu 265 walikufa na maelfu walilazimika kuyahama makazi yao wakati wa miezi miwili ya mvua isiyokoma katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki.
Mvua za sasa za El Nino zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 15 nchini Kenyana kupoteza maisha ya wengine zaidi ya 20 katika mkoa wa Somali nchini Ethiopia.