1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Mafuriko yaitikisa China

Babu Abdalla23 Julai 2021

Watu kadhaa wameokolewa kwa kutumia madaraja ya muda leo Ijumaa kutokana na mafuriko katika maeneo ya katikati mwa China yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 51.

https://p.dw.com/p/3xw7J
TABLEAU Weltspiegel 21.07.21
Picha: AFP/Getty Images

Watu kadhaa wameokolewa kwa kutumia madaraja ya muda leo Ijumaa kutokana na mafuriko katika maeneo ya katikati mwa China yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 51. Wakati huo, kimbunga kinachotarajiwa kuipiga China siku ya Jumapili kinatishia kufanya uharibifu zaidi na kuvuruga mipango ya uokoaji. Katika ripoti ifuatayo, 

Mamilioni ya watu wameathirika na mafuriko katika mkoa wa Henan, ambayo kwa upande mwengine yamesababisha watu kukosa chakula na maji safi kwa siku kadhaa.

Idadi ya vifo kutokana na mafuriko hayo inatarajiwa kuongezeka, huku maafisa wa mkoa wakiwaambia waandishi wa habari leo Ijumaa kuwa idadi ya majeruhi bado inahesabiwa.

Soma zaidi: Mkakati wa China kudhibiti idadi ya watu wa Xinjiang

Katika hali ambayo inatarajiwa kuongeza masaibu zaidi katika mkoa huo wa Henan, shirika la habari la serikali limesema kimbunga cha In-Fa kinatarajiwa kupiga mkoa huo katika muda wa siku chache zijazo na kuongezea mzigo zaidi kwa hali hiyo.

Katika mji ulioathirika zaidi na mafuriko hayo wa Zhengzhou, wazima moto wameendelea kuondoa maji yenye tope kutoka kwa mahandaki, ikiwemo njia ya chini kwa chini ambapo watu kadhaa walizama ndani ya gari moshi mapema wiki hii wakati kiwango cha mvua kinachoshuhudiwa kwa mwaka mzima, kilinyesha ndani ya siku tatu pekee.

Li Qiuhua, ni mkaazi wa Zhengzhou "Kwa kweli niliingiwa na hofu kidogo. Mimi natokea sehemu za kusini, na katika maisha yangu nimeona dhoruba kadhaa za mvua, nimeshuhudia majanga ya mvua katika mji niliokulia ila sijawahi kuona mfano wa janga hili. Hali imekuwa mbaya sana."

China Unwetter l Heftige Regenfälle, Überschwemmungen in Henan
Mvua zimesababisha mafuriko katika mji wa Zhengzhou, mkoa wa Henan. Picha: Hou Jianxun/HPIC/dpa/picture alliance

Mnamo usiku wa kuamkia leo, mvua kubwa ilisababisha mafuriko kuongezeka kaskazini mwa mji wa Xinxiang na viunga vyake, ambapo sehemu kubwa ya mashamba yalifurika maji baada ya mto Wei kuvunja kingo zake.

Idara ya hali ya hewa inasubiri kwa hali ya tahadhari kimbunga hicho cha In-Fa ambacho tayari kimesababisha mvua kubwa katika maeneo ya Taiwan na pwani ya mashariki ya China. Kimbunga In-Fa kinacharajiwa kupiga mnamo siku ya Jumapili, katika eneo la maakazi ya mamilioni ya watu.

Idara ya hali ya hewa imewaonya watu kujiandaa kwa mvua kubwa itakayokuwa na mchanganyiko wa upepo na mawimbi makali.

Maswali yameibuka juu ya jinsi China inavyoweza kujiandaa kukabiliana na hali mbaya za hewa, ambapo watalaamu wanasema majanga kama hayo ya mafuriko yanaongezeka kwa kasi kubwa duniani kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.