Mafuriko yaua watu 50 DRC
13 Desemba 2022Takriban watu 50 wamefariki katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Kinshasa baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosomba makaazi ya watu.
Picha zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo shirika la habario la Reuters halikuweza kuzithibitisha mara moja zimeonesha maeneo mengi ya mji huo yakiwa kwenye mafuriko na matope huku barabara zikipasuka.
soma pia:Je mabadiliko ya tabia nchi yamechangia mafuriko?
Video moja iliyonesha barabara kuu ya eneo hilo ikipasuka katikati na kuacha shimo kubwa lilosababisha magari chungunzima kutumbikia katika wilaya ya Mont-Ngafula.
Watu waliokuwa karibu wakishuhudia walionekana wakitafuta maeneo ya pembeni kujinusuru.Mkuu wa polisi Sylviano amesema kiasi watu 50 wamefariki kufuatia mafuriko hayo na idadi hiyo inaweza kuongeza.
Waziri mkuu na gavana wa mkoa huo wanatembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko na maafisa wa eneo hilo wanatarajiwa kukutana na wawakilishi wa wizara ya mambo ya ndani na vyombo vingine vya dola kulishughulikia suala hilo la dharura.
Kinshasa ambao uliwahi kuwa na vijiji vya uvuvi katika ukingo wa mto Congo umegeuka kuwa moja ya miji mikubwa kabisa ukiwa na wakaazi kiasi milioni 15.
Hata hivyo mifumo mibovu ya mpangilio wa mji huo uliokuwa kwa kasi umeifanya Kinshasa kuzidi kuwa katika hatari ya kukabiliwa na mafuriko baada ya mvua za mfululizo ambazo zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kiasi watu 39 walifariki mnamo mwaka 2019 kufuatia mvua za msimu zilizosababisha mafuriko katika wila kadhaa za mji huo na baadhi ya majengo kuporomoka barabara kuharibiwa vibaya.